MANCHESTER, England
KOCHA wa zamani wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson, amemtaka kocha wa sasa wa klabu hiyo, Jose Mourinho, kuwapa nafasi wachezaji vijana kwa ajili ya mafanikio ya baadaye.
Ferguson amedai kwamba utamaduni wa klabu hiyo ni kuwatumia vijana chipukizi ili kukomaza wachezaji hao ambao wataweza kuitumikia klabu kwa kipindi kirefu.
Kocha huyo amedai kwamba kuna vijana wenye umri mdogo ndani ya klabu hiyo kama vile, Marcus Rashford, Axel Tuanzebe, Tyrell Warren na Jesse Lingard, wachezaji hao wameonesha uwezo wao mkubwa hivyo wanaweza kuwa nyota zaidi kwa misimu ijayo.
“United ina uwezo wa kufanya makubwa katika michuano ya Ligi Kuu nchini England, muda sasa haijafanya vizuri lakini uwezo wa kufanya hivyo inawezekana.
“Kikubwa ni kuwapa nafasi wachezaji ambao wamesajili na wale ambao wapo, ninaamini kuna uwezekana mkubwa wa kufanya vizuri kama vijana hao watapewa nafasi ya mara kwa mara kwa ajili ya kuzoea ushindani uliopo.
“Wakati naifundisha timu hiyo nilikuwa nawapa nafasi vijana kwa kuwa niliamini wanaweza kuwa kwenye kikosi kwa muda mrefu,” alisema Ferguson.
Hata hivyo, kocha huyo amedai kwamba anaamini Mourinho anaweza kubadilisha soka na kuwa la kisasa zaidi kutokana na kushuka kwa miaka ya hivi karibuni.
“Mourinho ni kocha mzuri, ana uwezo mkubwa na ana historia ya kutwaa mataji katika klabu mbalimbali, hivyo ninaamini hata Manchester United anaweza kufanya hivyo kama alivyofanya katika klabu nyingine.
Hata hivyo, Mourinho mwenyewe ameahidi makubwa ndani ya klabu hiyo hasa katika kuhakikisha timu hiyo inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2017.
Kocha huyo tayari amefanya usajili kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, kama vile kwa kumnasa aliyekuwa mshambuliaji wa PSG, Zlatan Ibrahimovic na wengine.
Bado kocha huyo anaendelea kufanya usajili ambapo kwa sasa wanamtazama nyota wa klabu ya Juventus na timu ya taifa ya Ufaransa, Paul Pogba, huku kocha huyo akidai kuwa tayari kuachana na wachezaji wake wanane kwa ajili ya kufanikisha usajili wa mchezaji huyo.