NA ADAM MKWEPU,
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeitoza faini ya dola za Marekani 10,000 (Sh milioni 21.4) klabu ya Yanga kutokana na vurugu za wachezaji wake na kumzonga mwamuzi wakati wa mchezo wa marudiano hatua ya 16 bora Kombe la Shirikisho dhidi ya Sagrada Esperanca nchini Angola, Mei 18, mwaka huu.
Uamuzi huo ulitolewa jana kufuatia kikao cha Kamati ya Nidhamu ya CAF kilichofanyika Julai 3 mwaka huu mjini Cairo, Misri.
Katika mchezo huo, Yanga ilifungwa 1-0 lakini ikafuzu hatua ya makundi Kombe la Shirikisho kwa jumla ya mabao 2-1 kufuatia ushindi wa mabao 2-0 mchezo wa awali uliopigwa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, Yanga wanatakiwa kulipa dola 10,000 za Marekani ambapo dola 5,000 zinaweza kurejeshwa kwa klabu hiyo kwa sharti la kutofanya kosa hadi mwisho wa Kombe la Shirikisho mwaka 2016.
Adhabu nyingine ilikuwa ya Mo Bejaia ya Algeria ambayo ilitozwa faini ya dola 10,000 za Marekani baada ya mashabiki wake kufanya vurugu katika mchezo dhidi ya Yanga Juni 18, nchini Algeria.
Mchezo mwingine wa Kombe la Shirikisho kwa Yanga ni Jumamosi hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Medeama ya Ghana.