Peter Fabian na Sheila Katikula-MWANZA
MTUHUMIWA wa mauaji ya watu watatu ndani ya Msikiti wa Rahmani eneo la Ibanda relini, ametoroka akiwa chini ya ulinzi wa polisi katika mlima wa Kiloleli eneo la Nyasaka wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Mtuhumiwa huyo ambaye pia anahusishwa na ujambazi katika maduka yanayojishughulisha na miamala ya fedha, alitoroka wakati alipowapeleka polisi kuwaonesha watuhumiwa wenzake walipojificha.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema mtuhumiwa Hamisi Juma (38) mkazi wa Nyegezi alifanikiwa kuwatoroka askari wa upelelezi aliokuwa amewapeleka kuwaonyesha wahalifu wenzake walipojificha ndani ya mapango.
“Tukio hili lilitokea Julai 3, mwaka huu saa 2:00 usiku, mtuhumiwa, Hamisi Juma, akiwa chini ya ulinzi wa polisi wa upelelezi, aliwapeleka kuwaonyesha eneo jingine wanapojificha watuhumiwa wa ujambazi katika kilima cha Kiloleli-Nyansaka, baada ya kufika ghafla eneo la tukio majambazi waliokuwa wamejificha walifyatua risasi kuwashambulia askari.
“Askari wakiwa na taharuki na kuanza kujibu mashambulizi, mtuhumiwa alipata mwanya wa kuwatoroka askari, alielekea eneo jingine la mlima na kuwaacha askari wakiendelea kurushiana risasi.
“Tunaendelea kumsaka Hamisi na wenzake ambao walipata mwanya wa kukimbia kusikojulikana. Askari wetu walifanikiwa kukamata bunduki moja aina ya Shortgun iliyokatwa mtutu na kitako, ikiwa na risasi moja,”alisema.
Alisema polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine wa mauaji ya msikitini na ujambazi wa kutumia silaha kwenye maduka na vibanda vya miamala ya fedha, Mohamed Bishof (31) mkazi wa Nyasaka ambaye aliruka kutoka ndani ya gari la polisi na kuanguka barabarani kwa lengo la kutoroka ambapo aliumia kichwani na sehemu mbalimbali ya mwili wake.
“Mtuhumiwa Bishof alifariki dunia akiwa njiani wakati anapelekwa hospitali kupatiwa matibabu. Wakati wa uhai alipohojiwa alikiri kushiriki matukio ya mauaji ya watu watatu katika msikiti wa Rahman na matukio ya unyang’anyi kwenye maduka ya fedha.
“Huyu tulimkamata akiwa na kompyuta mpakato (Dell) ambayo aliipora kwenye tukio la ujambazi Kishiri Center Mei 5, mwaka huu,” alisema.