Na Mwandishi Wetu, Dodoma
HAPA ni kipigo tu. Hayo ni maneno ya wauguzi wa Hospitali ya Mirembe ambayo hutibu wagonjwa wa akili.
Hospitali hiyo kubwa na maarufu nchini kwa kutibu wagonjwa wenye matatizo ya akili iliyopo mkoani Dodoma, hali sasa imebadilika.
Wauguzi wa hospitali hiyo wanasema licha ya kazi ngumu inayoambatana na vipigo, wamekuwa hawapewi fedha za gharama za matibabu.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema wamekuwa wakikabiliana na hali hiyo ikiwemo ya kupigwa na wagonjwa pindi wanapokuwa wanawahudumia.
Watumishi waliotajwa kupata vipigo vya wagonjwa ambao walijeruhiwa katika maeneo mbalimbali ya miili yao ni Samwel Sumbuko ambaye alivunjwa mbavu mbili kwa kupigwa ngumi, Jackson Marco, aliyevunjwa mkono na Sara Mwakapusya alijeruhiwa paja.
Wengine ni Regina Kinyaiya aliyeng’atwa kidole, Stella Lutete aliyeng’atwa pamoja na Asia Kilingo, ambaye alipigwa na kupasuliwa kichwani wakati akimhudumia mgonjwa hospitalini hapo.
“Tunapigwa, hatulindwi, hatusikilizwi, hatulipwi gharama za matibabu na hata tukimfuata mkurugenzi anakujibu majibu mabaya. Na sasa imefika mahali wale wagonjwa wakorofi tunalazimika kuwakwepa kabisa.
“Hii kazi inahitaji moyo sana, lakini kwa kuwa ndiyo taaluma yetu tuliyosomea hatuna budi, ila kiukweli tupo katika wakati mgumu sana, unatoka nyumbani ukiwa mzima na ukirudi unaweza kujikuta huna meno au hata kuvunjwa mguu,” alisema mmoja wa watumishi wa hospitali hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alisema wanalazimika kukwepa kuwahudumia wagonjwa wakorofi kama njia ya kunusuru maisha yao, lakini bado uongozi umekuwa hauliangalii suala hili kwa uzito.
“Magufuli (Rais Dk. John) si yupo kwa ajili ya wanyonge, sisi wafanyakazi wa Mirembe tunafanya kazi katika mazingira magumu sana na sababu ni Mkurugenzi na Katibu wake wameifanya hospitali hii ni shamba la bibi.
“Suala la wafanyakazi kutolipwa fidia kwa muda mrefu baada ya matukio ya kupigwa, kuumizwa na kung’atwa na wagonjwa wa akili kwetu limekuwa ni tanuru la mateso kwani pamoja na kujaza fomu za kuomba malipo lakini utaambuliwa majibu mabaya na kutolipwa kabisa.
“… na haya yote yanatokana na mkurugenzi wa hospitali hii (Mirembe), ambaye amekuwa hata akitufanya tushindwe kufanyakazi kwa moyo. Tunashindwa kuelewa sijui tumemkosea nini Mungu—– (kilio), Magufuli njoo na hata kwetu usikie kilio chetu nasi,” alisema mtumishi huyo huku akibubujikwa na machozi.
Alisema pamoja na hali hiyo, Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Erasmus Mndeme, amekuwa akiwadhalilisha mbele ya wagonjwa na ndugu zao bila kujali utu na hali ya mtumishi.
“Inafika mahali wagonjwa wakati mwingine wamekuwa wakituheshimu lakini ikitokea mkurugenzi ukamweleza suala la mgonjwa anahitaji kitu fulani utapata majibu ambayo hutayasahau,’’ alisema.
Muuguzi mwingine alisema pamoja na hali hiyo, wamekuwa hawalipwi stahiki zao kwa muda mrefu zikiwemo za malipo ya utendaji wa muda wa ziada na mazingira hatari na kutokuwepo kwa uwazi wa matumizi ya fedha za maendeleo.
Alisema muuguzi mmoja kwa siku anahudumia wagonjwa zaidi ya 100 wenye matatizo ya akili, jambo ambalo ni hatari.
“Mazingira haya si rafiki kwani wagonjwa wa akili wengine ni wakorofi na wengine hutaka kuwapiga hivyo kushindwa sehemu ya kukimbilia. Kuna wodi A, B na D ambazo hutakiwa kuingia muuguzi mmoja jambo ambalo ni hatari sana,” alisema.
Muuguzi huyo alitolea mfano tukio lililotokea Juni 19, mwaka huu na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, mgonjwa Stella Mbalwa, alimpiga na kumuua mgonjwa mwenzake, Halima Chedi kwa ubao kutokana na kugombea uji.
Alisema kitendo hicho ni cha hatari kwani huwafanya waishi kwa hofu huku wakihofia usalama wa maisha yao.
“Tunahudumia hapa lakini hadi sasa unaweza kuamini kwamba hatuna hata kadi ya matibabu ya bima ya afya kama ilivyo mahali pengine pa kazi. Hii taasisi ipo chini ya Serikali ila haipewi kipaumbele.”
Licha ya hali hiyo alisema kuwa wagonjwa hao wa akili kwa muda sasa wamekuwa wakipewa vyakula na hospitali, lakini wengi wao hudhoofika kwa kukosa vyakula vyenye vitamin inayotakiwa kwa binadamu.
Kutokana na hali hiyo ilielezwa kuwa wagonjwa hao hutakiwa kula wali na nyama mara mbili kwa wiki huku siku nyingine wakitakiwa kupatiwa wali na maharage na mboga za majani.
“Inaumiza sana, ni muda mrefu wagonjwa wamekuwa wakila ugali na maharage pamoja na uji usiokuwa na sukari mpaka mkurugenzi aamue ndiyo wale wali. Nakwambia hivi kuna siku waligoma (wagonjwa) wakitaka na wao wale wali na nyama, nakumbuka ilikuwa siku ya Pasaka mwaka jana,” alisema muuguzi huyo.
MTANZANIA lilipokwenda ofisini kwa Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Erasmus Mndeme, ili kupata ufafanuzi wa madai hayo aligoma kutoa ufafanuzi huku akimtaka mwandishi atoke ofisini kwake.
“Nyie waandishi mnataka msikilizwe nyie tu sasa hivi nina mambo yangu nayaandaa hivyo naombeni mtoke ofisini kwangu, nikimaliza nitawapigia,” alisema Dk. Mndeme.
Kutokana na majibu hayo gazeti hili lilimtafuta Naibu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla, ili kupata maelezo ya Serikali kuhusu madai ya wauguzi hao ambapo alisema hana taarifa za kina kuhusu madai hayo, huku akiahidi kufuatilia ili kujua ukweli.