29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaji mahakama ya mafisadi mafunzoni

Mohamed Othmani Chande
Mohamed Othmani Chande

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam

BAADA ya Bunge kupitisha marekebisho ya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 ya mwaka 2002 na kuanzisha mahakama ya mafisadi, Jaji Mkuu, Mohamed Othmani Chande, amesema wapo mbioni kutunga kanuni za uendeshaji wa mahakama hiyo.

Pia amesema tayari mchakato  wa ujenzi wa majengo ya mahakama hiyo umeanza na maandalizi ya majaji, ambapo majaji 14 wa Mahakama Kuu wataanza mafunzo Julai 11 hadi 15 mwaka huu katika Chuo cha Sheria Lushoto, Tanga.

Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mabanda ya Mahakama ya Tanzania katika maonesho ya kimataifa ya biashara yanayoendelea kwenye viwanja vya Sabasaba vya Julius Nyerere.

“Wakati Rais anaidhinisha marekebisho ya sheria yaliyopitishwa na Bunge, matakwa ya sheria yananitaka nitunge kanuni za sheria hiyo zitakazoelezea mambo mabalimbali kama vile kanuni za kufungua masijala na kanuni za kulinda mashahidi hivyo tuko mbioni kutunga kanuni hizo, ” alisema Jaji Chande na kuongeza:

“Mashauri yanayohusu rushwa, uhujumu uchumi na ugaidi yanataka kanuni nzuri za namna ya kuwalinda mashahidi ili wasipate athari za kesi hizo,” alisema.

Alisema mafunzo yatakayotolewa kwa majaji hao yanalenga kuwajengea uwezo wa kuendesha kesi kwa haraka na kwamba kesi moja haitadumu zaidi ya miezi tisa.

“Zile kesi ambazo ushahidi utakuwa umekamilika hatutaki zidumu mahakamani kwa zaidi ya miezi 9…hizi ni jitihada ambazo zinafanywa hata kwa mahakama nyingine kwa sababu tumepokea maoni ya wananchi wanasema wanakerwa na ucheleweshwaji wa kesi na wengi wanasema bora kesi iwahishwe kuliko kuamuliwa sawa, ” alisema Jaji Chande.

Alisema majengo ya mahakama ya mafisadi yatajengwa pembeni ya Shule ya Sheria Tanzania iliyopo Sinza Wilaya ya Kinondoni na tayari wathamini wameshaanza kazi.

Akizungumzia maboresho ya utendaji wa mahakama nchini alisema zimeandaliwa simu zaidi ya 350 ambazo wananchi watazitumia kutoa malalamiko yao kuhusu mwenendo wa mahakama pamoja na kutoa maoni ya namna ya kuboresha.

Alisema kutakuwa na simu kwenye mahakama za hakimu mkazi za wilaya na simu maalumu kwenye ofisi za wilaya za TAKUKURU na katika ofisi za mkuu wa wilaya ambazo zitakuwa zinapokea malalamiko kuhusu mahakama.

Aliongeza kuwa maboresho hayo yanaenda sambamba na ujenzi wa majengo ya mahakama ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita zilitengwa sh bilioni 12.3 ambazo zitajenga mahakama 10 za wilaya, mahakama kumi za mwanzo na ukarabati wa mahakama 15.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles