NA ZAITUNI KIBWANA, DAR ES SALAAM
TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, imejiwekea mazingira mazuri ya kusonga mbele katika michuano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa za Afrika ya Vijana (Afcon 17), baada ya jana kuichakaza  Shelisheli kwa kuifunga mabao 3-0.
Kikosi cha Serengeti Boys chenye historia ya kufanya vizuri katika mechi za kimataifa za kirafiki walizocheza, ndio waliotawala zaidi mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo wa jana ulianza kwa kasi huku wenyeji Serengeti Boys wakiwa na uchu wa kupata bao la mapema ambapo dakika ya pili, Asad Juma, alitoa pasi safi kwa Ally Msengi, lakini alichelewa kuufikia mpira ambao uliokolewa na kipa wa Shelisheli.
Dakika ya 15 Serengeti Boys walipata bao la kwanza kupitia kwa Nickson Kibabage aliyemalizia mpira wa kona iliyochongwa na  Asad.
Asad ambaye aling’ara katika mchezo wa jana na kuwavutia mashabiki wengi waliojitokeza uwanjani, alitoa pasi safi kwa Kelvin Naftal dakika ya 20 lakini alishindwa kuitumia nafasi hiyo baada ya mabeki wa Shelisheli kuwahi kuokoa hatari hiyo.
Bao la pili kwa Serengeti Boys lilipachikwa wavuni dakika ya 22 mfungaji akiwa ni Ibrahim Ali ambaye alimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Shelisheli wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa.
Dakika ya 33, Serengeti walikosa nafasi ya wazi ya kufunga baada ya Kibabage kutoa pasi fupi iliyomkuta Ibrahim Ali ambaye alifanya uzembe na kutoa nafasi kwa mabeki wa Shelisheli kuokoa hatari hiyo.
Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Serengeti Boys waliotawala kwa dakika zote 45 wakiongoza kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Serengeti kufanya mabadiliko ya kumtoa Naftal na nafasi yake kuchukuliwa na Cyprian Mtasingwa dakika ya 46, mabadiliko ambayo yaliongeza kasi ya mashambulizi kwa wapinzani wao.
Dakika ya 61, Msengi aliipatia bao la tatu Serengeti Boys kwa mkwaju wa penalti baada mchezaji wa Shelisheli kuunawa mpira eneo la hatari wakati wa kuokoa mpira wa adhabu uliopigwa na Kibabage.
Dakika ya 72, Serengeti Boys walifanya mabadiliko ya kuwatoa Asad, Israel Mwenda kuwaingiza Erick Nkosi na Mohammed Abdallah huku Shelisheli wakimtoa Hegled Havelock na kuingia Deema Durel.