NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
SAFU ya ushambuliaji ya timu ya Yanga ni kama imepata mtikisiko wakati ikijiandaa kuvaana na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kesho katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya mastraika tegemeo, Donald Ngoma na Amissi Tambwe kuzichapa mazoezini.
Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa wamejichimbia kambini nchini Uturuki kujiandaa na mchezo huo muhimu wa Kundi A katika Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Kitendo hicho cha utovu wa nidhamu kwa nyota hao, kimetokea wakati kikosi hicho kikiwa kinajipanga kukaa sawa kwenye michuano hiyo baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria ugenini kwa kukubali kipigo cha bao 1-0.
Akizungumzia suala hilo, Tambwe alilithibitishia MTANZANIA kutokea kwa tukio hilo mazoezini na kudai kwamba alishangazwa na kitendo cha mshambuliaji mwenzake kumvamia na kuanza kumshambulia.
“Hakuna juhudi zozote zilizochukuliwa na uongozi ili kumaliza tatizo hili, kwani Ngoma anaonekana kuwa ana bifu dhidi yangu kwa muda mrefu sasa, sioni sababu yoyote ya kunipiga, binafsi sijapendezwa na kitendo alichonifanyia.
“Najua sitacheza dhidi ya TP Mazembe kwa sababu nina kadi mbili za njano, lakini kitendo hiki hakikupaswa kufanyika na hakuna sababu ya jambo hilo kutokea kwani sisi wote tunataka timu yetu ifanikiwe,” alisema Tambwe.
Katika tukio hilo, Tambwe aliumia vibaya na kulazimika kukimbizwa hospitalini ambako alipatiwa matibabu na kushonwa nyuzi tatu sehemu aliyopasuka.
Hata hivyo, straika huyo raia wa Burundi hakutaka kuweka wazi chanzo cha ugomvi uliopelekea kupigana hadharani na kudai aulizwe Ngoma ndiye anayejua sababu ya kufanya hivyo.
Juhudi zilizofanywa na gazeti hili kumpata Ngoma ili kuelezea chanzo cha ugomvi wao ziligonga mwamba kutokana na kutopatikana kwenye simu ya mkononi.