32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kitwanga: Yaliyotokea namwachia Mungu

Charles Kitwanga*Asema amerudi na nguvu mpya, kutua bungeni wiki ijayo

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amesema yupo imara na amerejea nchini akiwa na matumaini mapya.

Pamoja na hali hiyo, amesema kuwa hivi sasa anajipanga kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha anaisaidia nchi pamoja na wapigakura wake na kuwa na maendeleo ya kweli na Jumatano ya Julai 29, ataripoti bungeni.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu, baada ya kurejea akitokea nchini Israel ambako alikwenda kwa shughuli zake binafsi.

Alisema licha ya mtihani uliomkuta, kwa sasa yupo imara kwa ajili ya kuwatumikia wapigakura wake kwa kuwawakilisha vema ndani ya Bunge.

“Niko imara kabisa na nina nguvu na matumaini mapya, nimeingia nchini jana (juzi) nikitokea nchini Israel ambako nilikuwa na shughuli zangu binafsi. Unajua mimi ni mtaalamu (wa mawasiliano) na wewe unajua kabla sijaingia kwenye siasa nilikuwa nafanya nini.

“Kifupi ninasema nilikwenda Israel kwa shughuli zangu binafsi kabisa ambazo kwa kipindi cha wiki tatu nilizokuwa huko nimefanya. Hata wanaosema nilikwenda kulia kwa Bwana nao ni mawazo yao, maana unajua ile ni nchi takatifu kutokana na historia yake,” alisema Kitwanga.

Alipoulizwa amepokeaje hatua ya kufutwa kwake kazi na Rais John Magufuli kwa kile kilichoelezwa ni ulevi, alisema kwa sasa hawezi kusemea jambo hilo kwani aliyemteua ndiye mwenye mamlaka ya kumwajibisha.

“Rais ni mtu mkubwa anaweza kufanya jambo lolote ili mradi havunji sheria, hata kilichotokea kwangu ni mamlaka yake halali, ingawa Mungu ndiye muweza wa kila jambo. Mimi ni Mkristo safi, nasi tumefundishwa kusamehe saba mara sabini na kusahau yaliyopita,” alisema.

Akieleza mikakati yake, Kitwanga alisema kuwa baada ya kuripoti bungeni wiki ijayo, atakuwa na ziara ya wiki tano ndani ya jimbo lake ambako atazungumza na wapigakura wake na kueleza yaliyomsibu hatua kwa hatua.

“Sitaki kuingia ndani sana ila mengine nitayasema nikiwa jimboni, lakini si kwa lengo la kubishana na mtu, na uzuri kila hatua ambayo nimepitia hata wapigakura wangu walikuwepo kwa uwakilishi wa madiwani wa Misungwi ambao walikuwa mjini Dodoma,” alisema.

Mei 21, mwaka huu, Rais Magufuli alimng’oa Kitwanga kuhudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kutokana na madai ya ulevi, huku taarifa zaidi za ndani zikieleza kuwa alianza kushughulikiwa bila yeye mwenyewe kujua.

Pamoja na uamuzi huo wa Rais Magufuli, imeelezwa kuwa Kitwanga pamoja na timu yake walikuwa wakifuatiliwa nyendo zao na makachero.

Chanzo cha kuaminika kililiambia gazeti hili kuwa moja ya taarifa ambazo ziliwasilishwa kwa Rais Magufuli ndiyo iliyomlazimu kuchukua hatua hiyo.

“Unajua Kitwanga alikuwa akishughulikiwa muda mrefu bila yeye mwenyewe kujua, na hata kuondolewa kwake hadi sasa haamini. Wapo walioeleza kuwa baada ya kuwasilisha bajeti yake Mei 16, mwaka huu, alikwenda kulala Morogoro badala ya nyumbani kwake mjini Dodoma katika eneo la Sengia (Site11).

“Lakini pia inadaiwa kwamba kwa muda amekuwa halali nyumbani kwake na kwenda katika moja ya hoteli (jina linahifadhiwa) mjini Dodoma ambako hulewa hadi asubuhi jambo ambalo si la kweli, ni kama mkakati wa kumshughulikia na si hivyo tu hata baadaye zilitolewa taarifa kuwa yupo Morogoro ambako pia watu walimfuatilia kwa karibu, lakini kwa bahati nzuri hakuwepo.

“Tena si hilo tu, hata pia eti wanadai alilewa sana kwa kunywa Vodka hali ya kuwa hatumii kinywaji hicho na bila kujijua tangu usiku alipokuwa na madiwani wake yaani Mei 19, alikuwa akifuatiliwa na vyombo vya dola, tena walikuwa wakitumika wanawake ambao kama ndio walikuwa wakiandaa taarifa mbaya dhidi yake,” alisema mtoa habari wetu ambaye yupo karibu na mbunge huyo wa Misungwi.

Chanzo hicho cha habari kilisema kuwa pamoja na hali hiyo, wapo baadhi ya vigogo kutoka katika mashirika na taasisi nyeti za Serikali ambao walikuwa na vita ya kufa na kupona dhidi ya Kitwanga, hadi kufikia kufanya vikao vya siri vya kumshughulikia.

Kilisema kuwa mipango hiyo ilipangwa kwa ustadi mkubwa, na kwamba tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, kuna baadhi ya watu walikuwa wakimfutilia kwa karibu wakiwemo ndani ya idara zilizokuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

“Unajua huyu bwana alianza kushughulikiwa muda kidogo tangu siku ilipotolewa taarifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, iliyoeleza kwamba naye hakujaza fomu ya maadili ya viongozi wa umma, yeye pamoja na mawaziri wenzake akiwemo Balozi Augustino Mahiga na January Makamba, ingawa nguvu kubwa ilikuwa kwake.

“Na tangu wakati huo haukupita muda kidogo likaibuka suala la Lugumi na kama unakumbuka hapo alikuwa na vita ndani ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na Uhamiaji ambako kote huko kuna watu waliwajibishwa,” alisema mtoa habari wetu.

Pamoja na hali hiyo, katika kile ambacho kilikuwa kikiwatesa baadhi ya watu ndani ya Serikali, ni hatua ya ukaribu kati yake na Rais Magufuli ambao kuna wakati zilisambazwa video katika mitandao ya kijamii zikimuonyesha akiwa na kiongozi huyo wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi katika Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Katika video hiyo anaonekana Kitwanga akiwa na Rais Magufuli katika moja ya uwanja wa ndege ambako alikuwa akimuhamasisha achukue fomu ya kuwania urais, jambo ambalo alitekeleza baadaye na kufanikiwa kupita katika mchujo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles