32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Afrika ina kila sababu za kukaribisha wawekezaji wakubwa  

wsMOJA ya vitu vilivyowabeba wagombea urais nchini Marekani ni ahadi ya kurudisha viwanda na kuvunja mikataba ya kibiashara inayochangia ukosefu wa ajira kwa vijana wengi nchini humo.

Kwa kufanikiwa kuwachota vijana wengi si tu wale wasio na ajira bali pia na wengine wa kipato kidogo, waliweza kutamba katika hatua hiyo ya mchujo na kuwashangaza wengi wakiwamo wafuatiliaji wa siasa ndani na nje ya taifa hilo.

Ninaowazungumzia katika utangulizi huo hapo juu si wengine zaidi ya bilionea Donald Trump, ambaye tayari amejihakikishia tiketi ya kukiwakilisha Chama cha Republican katika uchaguzi wa rais utakaofanyika Novemba mwaka huu pamoja na Bernard Sanders wa Chama cha Democratic.

Sanders licha ya umri wake wa miaka 71 na ingawa ameikosa tiketi ya kuwania urais, alipata mafanikio kwa kuzoa kura za mamilioni ya vijana na hivyo kumwendesha mchakamchaka na kumnyima raha chaguo la vigogo Hillary Clinton, ambaye tayari amejihakikishia tiketi ya kuiwakilisha Democratic.

Naam, hawakuwa na nafasi walau kuwa tishio kwa vile Trump kwa mfano; amejijengea maadui wengi miongoni mwa makundi tofauti ya wapiga kura nchini humo kutokana na kauli zake tata na za kibaguzi huku Sanders akiwa ametokea kusikojulikana.

Lakini uwezo wao wa kujenga hoja pamoja na mvuto wa haiba yao kwa kadiri ya mchakato wa kura za mchujo ulivyoendelea ndivyo walivyoweza kujiongezea wafuasi hasa kutokana na misimamo yao kadhaa ikiwamo hilo la kuahidi kuvirudisha viwanda vya Marekani kwa masilahi ya taifa na Wamarekani.

Wote wawili wameshutumu utawala wa sasa na zilizopita pamoja na mambo mengine; kwa kulinda au kuingia mikataba ya kibiashara iliyoshuhudia viwanda vikihamia ng’ambo hususani Asia.

Wana mtazamo mmoja kwamba mikataba hiyo imesababisha ukosefu mkubwa wa ajira nchini humo huku taifa hilo likigeuka dampo la bidhaa za nje hasa kutoka China.

Kwa msingi huo wawili hao wanaonwa kama watetezi wa wanyonge huku wagombea wengine wa karba ya Clinton wakihesabiwa ‘marafiki’ wa wafanyabiashara wakubwa ambao wanaangalia manufaa yao binafsi bila kujali ya taifa hilo kwa mapana.

Tukiachana na siasa hizo, ambazo si makusudio yetu ya makala haya na bila kuchambua au kulinganisha faida au hasara kwa taifa pale mwekezaji wake anapoamua kwenda ng’ambo, ni ukweli usiopingika kuwekeza kwingine hasa kwenye gharama ndogo za uendeshaji kunazalisha faida kubwa mno.

Kwa sababu hiyo, wawekezaji wengi wakubwa wa Marekani wanaangalia ng’ambo zaidi hususani barani Asia kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo soko na gharama ndogo za uendeshaji.

Ni gharama kubwa kuendesha kiwanda nchini Marekani kulinganisha na Asia hususani linapokuja suala la ulipaji mishahara. Kwa sababu hiyo, ili kupata faida kubwa baada ya kuondoa gharama za uendeshaji wawekezaji hukimbilia Asia.

Mathalani, kwa upande mwingine wawekezaji hubuni na kutengeneza bidhaa zao kama zile za kielektroniki nchini Marekani lakini baada ya hapo zinaenda kuunganishwa nchini China.

Hii yote imelenga kuzifanya bidhaa hizo zibakie au ziwe na sifa ya ubora wake unaotambulika kutokana na teknolojia ya juu iliyopo Marekani lakini pia kwa sababu ya kuhitaji faida kubwa huziunganisha ng’ambo ili kupunguza gharama na hivyo kutengeneza faida kubwa.

Hakuna ubishi China inabakia kuwa eneo mashuhuri zaidi kwa uwekezaji wa viwanda duniani ikivutia uwekezaji wa mamia kwa mabilioni ya dola kila mwaka.

Lakini kwa sababu ile ile ya gharama, China nayo sasa gharama za uendeshaji zinaelekea kupaa na kwa sababu ile ile ya kutafuta faida nono, wawekezaji wakati wakipanua uwekezaji wao wanaelekeza macho maeneo mengine ya Asia nje ya China, kama vile Vietnam, Thailand na kwingineko.

Miongoni mwa vitu vinavyowatia hofu wawekezaji nchini humo ni pamoja na mfumuko wa bei, uhaba wa wafanyakazi na nishati, kubadilika kwa sera za serikali na hata wasiwasi wa machafuko kutokea siku moja.

Lakini kitu muhimu zaidi kinachochangia wawekezaji kukimbia ni mishahara.

Nchini China mishahara imekuwa ikipanda kwa zaidi ya asilimia 25 kwa mwaka katika viwanda vingi kwa viwango vya dola ya Marekani na kuondoa ule unafuu wa China ambao hata hivyo huwezi kuulinganisha na mataifa ya magharibi.

Swali linalobakia kwa sasa baada ya Asia kuwa kimbilio la wawekezaji wengi wakubwa wa Magharibi kutokana na unafuu wa gharama za uendeshaji, je, Afrika kwa upande wake iko tayari kuwapokea wawekezaji wakubwa katika sekta mbalimbali ikiwamo utengenezaji magari na vifaa vya kielektroniki?

Afrika ina kila sababu ya kuwa kimbilio la wawekezaji hao kwa sababu mbalimbali ikiwamo gharama nafuu kulinganisha na Asia pamoja na soko la kujidai.

Mataifa mbalimbali ya Afrika katika harakati zake za kuelekea uchumi wa kati, uwekezaji katika sekta ya viwanda umekuwa kipaumbele chake kikuu.

Kwa mujibu wa tafiti sekta ya viwanda ndiyo hasa inayoshikilia ufunguo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutengeneza ajira kulinganisha na sekta nyingine.

Lakini kuna changamoto nyingi zinazokwamisha ndoto au kuchelewesha malengo yaliyokusudiwa.

Miongoni mwao ni ukosefu wa sera madhubuti zinazolenga kuboresha na kuendeleza sekta ya viwanda, udhaifu wa usimamizi na miundombinu ya barabara, reli, bandari na kadhalika pamoja na uhaba wa nishati ya kutosha.

Iwapo changamoto hizo zitashughulikwa ipasavyo hakuna kitakachoizuia wawekezaji wakubwa kuelekeza macho Afrika kutokana na faida kubwa watakayopata achilia mbali kwa mataifa yenyewe ya Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles