NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA
WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia na wengine sita wamelazwa hospitalini baada ya kula nyama ya ng’ombe inayodhaniwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa kimeta.
Sambamba na watu hao, mbwa na paka waliokula utumbo wa ng’ombe huyo baada ya kuchinjwa nao wamekufa.
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda ya Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, katika taarifa aliyoitoa jana kwa waandishi wa habari.
Akizungumza ofisini kwake jana, Kamanda Mambosasa alisema tukio hilo lilitokea Mei 28 mwaka huu katika Kijiji cha Mwaekesabe, Kata ya Kimaha, Wilaya ya Chemba iliyopo Mkoa wa Dodoma.
Kamanda Mambosasa aliwataja waliofariki kuwa ni Haji Nchalo mwenye umri wa miaka 20 na watoto mapacha, Yasir na Yasini waliokuwa na miaka saba.
“Tunahisi hawa wamekula nyama yenye kimeta ila uchunguzi bado unaendelea. Mtu wa pili ndiye alitupa taarifa lakini wenyewe walikuwa wanaficha,” alisema Kamanda Mambosasa.
Akizungumzia tukio hilo, Baba mzazi wa marehemu hao, Salum Nchalo ambaye naye amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma baada ya kula nyama hiyo, alisema yeye na familia yake nzima waliila baada ya kupewa na jirani yao.
Nchalo alisema alipewa nyama hiyo na jirani yake aliyemtaja kwa jina la Bakari Juma aliyemchinja ng’ombe wake baada ya kuonyesha dalili za kuwa mgonjwa.
Alisema yeye, mkewe pamoja na watoto wake saba waliila baada ya kupikwa lakini muda mfupi baadaye walianza kusumbuliwa na tumbo ambapo watoto wake watatu walifariki dunia huku yeye, mkewe na watoto waliosalia wakikimbizwa Hispitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.
“Nyama nilipewa na jirani yangu Bakari Juma ambaye alikuwa amewekeza ng’ombe kwa Iddi Kibure, Kibure alimletea ng’ombe huyo akidai anaumwa hivyo akaamua kumchinja kisha akatupatia na sisi nyama kwa ajili ya kitoweo,” alisema Nchalo.
Alisema mbali na wao, familia nyingine nane zilizopo katika kijiji hicho zilipewa nyama hiyo lakini anashangaa waliodhurika ni yeye na familia yake tu.
Nchalo alisema nyama hiyo kabla ya kuila ilioshwa vizuri kisha ikapikwa huku utumbo wakiwapa mbwa watatu na paka mmoja ambao baada ya kuula, siku iliyofuata waliwakuta wakiwa wamekufa.
“Ile nyama tuliyokula jioni utumbo tuliwapatia mbwa watatu na paka lakini asubuhi tuliwakuta wote wamekufa na sisi tukaanza kuharisha na kutapika ikabidi twende Zahanati ya Mwaekesabe wakasema hawana vipimo ndiyo ikatulazimu kuja huku Dodoma.
“Wa kwanza kuja hospitali ni watoto wangu mapacha ambao wamefariki. Mimi na mwanangu Haji tulikwenda Hosptali ya Mirembe lakini walipotuona tumezidiwa wakatuhamishia hapa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
“Mara baada ya kufika hapa tulipokewa vizuri lakini usiku wa juzi ndiyo Haji naye akafariki. Sasa nimebaki na watoto watano tu na mke wangu ambao sote tumelazwa hapa wodi namba 12,” alisema Nchalo.
Mganga wa zamu katika wodi namba 12 ambako familia ya Nchalo imelazwa, Rose Msigwa, alisema baada ya kuwapokea waliwapima lakini hawakuona tatizo lolote.
“Nitakupa jibu gani wao ndio wanatakiwa waseme wamekula nini, tumewapima vipimo vya kawaida na hakuna tatizo lolote, ila nenda kwa aliyewapokea atakupa jibu zuri mimi nimeingia jana sijui kinachoendelea,” alisema Msigwa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Zainabu Chaula, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo alisema yupo mbali na hospitali.