NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Jamal Malinzi, ameisifu bajeti ya shilingi bilioni tatu ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akidai kwamba inaweza kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya michezo nchini.
Bajeti hiyo iliwasilishwa juzi bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, wakati akisoma hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/17, iliyogharimu kiasi cha Sh trilioni 29.5 ikiwa ni ongezeko la Sh trilioni 7.01 kutoka bajeti ya mwaka 2015/16 iliyogharimu Sh trilioni 22.49.
Serikali ilitenga fedha hizo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya sanaa, ubunifu, utamaduni na michezo ikiwemo kuratibu na kusimamia uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Malinzi alisema kiwango cha fedha kilichotengwa kinatosha kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika michezo nchini.
“Bajeti nzuri hasa ikitumiwa vema kusaidia michezo kwa kipindi hiki ambacho timu za taifa zinakabiliwa na michuano ya kimataifa.
“Ingawa bado sijawa na taarifa kamili juu ya mgawanyo wa hizo fedha, lakini tunaishukuru Serikali kwa bajeti hii ambayo ni nzuri kwa upande wetu,” alisema Malinzi.
Aidha, bajeti hiyo ilikosolewa na baadhi ya wadau wa soka nchini, kwa madai ya kuegemea zaidi upande wa sanaa kuliko michezo hasa soka.