25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kununua ndege tatu mpya 2016/2017

Philip MpangoNa Khamis Mkotya, Dodoma

SERIKALI inakusudia kununua ndege tatu mpya   na meli moja mpya katika mipango ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2016/2017

Mpango huo umeelezwa jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, wakati akiwasilisha bungeni taarifa ya hali ya uchumi 2015 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/2017.

Dk. Mpango alisema Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2016/2017 umeainisha miradi mikubwa ya kielelezo ambayo itapewa msisitizo katika utekelezaji wake.

Dk. Mpango alisema  Serikali imekusudia kuimarisha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ikijumuisha ununuzi wa ndege tatu mpya.

“Moja ikiwa ni Bombardier CS300 yenye uwezo wa kubeba abiria 100 hadi 150 na dege mbili Bombardier Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 67 hadi 88 kila moja,” alisema.

Dk. Mpango alisema mpango huo unakwenda sambamba na uboreshaji wa usafiri katika maziwa makuu ikiwa ni pamoja na ununuzi wa meli moja mpya ya usafirishaji wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria na ukarabati wa meli za MV Victoria, MV Butiama na MV Liemba.

“Miradi hii ni mahususi kwa maana ya ukubwa wa uwekezaji na matokeo tarajiwa. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma, mradi wa chuma Liganga, ujenzi wa reli mpya ya kati Dar-Kigoma na Tabora-Mwanza hadi Msongati na Kaliua- Mpanda kwa kiwango cha standard gouge,” alisema.

 

Mwelekeo wa uchumi 2016/2017

Akizungumzia mwelekeo wa uchumi kwa mwaka 2016/2017, Dk. Mpango alisema malengo yake ni kuongeza pato la taifa kutoka asilimia 7.0 mwaka 2015 hadi asilimia 7.2 mwaka 2016.

“Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha   unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na asilimia 8.0 mwaka 2016.

“Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.8 ya pato la taifa mwaka 2016/2017 kutoka asilimia 12.6 mwaka 2015/2016.

“Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 23.2 ya pato la taifa mwaka 2015/2016 hadi asilimia 27.0 mwaka 2016/207.

“Nakisi ya bajeti inakadiriwa kuwa asilimia 4.5 ya pato la taifa mwaka 2016/2017 kutoka makadirio ya bajeti ya asilimia 4.2 mwaka 2015/2016.

“Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne ifikapo Juni 2017,” alisema.

 

Miradi iliyotekelezwa 2015/2016

Kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2015/2016, Serikali ilitenga Sh trilioni 5.909 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo kati ya hizo fedha za ndani zilikuwa Sh trilioni 4.246 na fedha za nje ni Sh trilioni 1.662.

Dk. Mpango alitaja miradi ya maendeleo iliyokamilika kama kielelezo cha mafanikio yaliyopatikana katika mwaka huo wa fedha kuwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja ya Kigamboni, Maligisu, Nangoo, Mbutu na Ruhekei katika barabara kuu.

“Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam (km 542). Ujenzi wa mitambo ya kuchataka gesi katika maeneo ya Madimba na Songosongo.

“Usimakaji wa mitambo minne ya kufua umeme Kinyerezi I yenye uwezo wa kuzalisha MW 150 na kuanza uzalishaji wa umeme,” alisema.

Kuhusu hali ya umasikini nchini, Dk. Mpango alisema Serikali inaendelea kuratibu na kufuatilia hali ya umasikini, ambako inaonyesha umasikini bado umetopea.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles