* Amtaka Magufuli kulinda Wazanzibari kwa gharama yoyote
* Asema Bunge limekuwa taasisi isiyojiamini
* Amshangaa Naibu Spika kwa kushindwa kutumia ualimu wake
NA ELIZABETH HOMBO KILWA
Kaskazini ni miongoni mwa majimbo yaliyopo mikoa ya Kusini yaliyokuwa yakiongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka mingi, ukiacha lile la Kilwa Kusini ambalo linaongozwa na Selemani Bundara maarufu ‘Bwege’ wa Chama cha Wananchi (CUF).
Pamoja na hilo, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana uliokuwa na hamasa kubwa na kubadilisha ladha ya siasa, baada vyama vya upinzani vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kuungana na kusimamisha mgombea mmoja kwa kila jimbo.
Ukawa kwa kiasi kikubwa umesaidia upinzani kuzoa majimbo mengi huku Vedasto Ngombale wa CUF akinyakua Jimbo la Kilwa Kaskazini lililokuwa likiongozwa na Murtaza Mangungu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ngombale ambaye ni (mtoto wa mdogo wake mwanasiasa mkongwe, Kigunge Ngombale Mwiru), alichaguliwa pia kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC). MTANZANIA imefanya mahojiano na Ngombale ambapo pamoja na mambo mengine anasema Ukawa ulikuwa injini ya ushindi wake Kilwa Kaskazini.
Endelea… SWALI: Hebu tueleze historia yako kwa ufupi kwa faida ya Watanzania JIBU: Nina umri wa miaka 41. Nilihitimu darasa la saba mwaka 1990 katika Shule ya Msingi Kipatimu.
Baadaye mwaka 1991 nikajiunga kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Kipatimu na kuhitimu mwaka 1994. Mwaka 1995 nikajiunga na Chuo cha Ualimu Nachingwea na nikahitimu mwaka 1997, baadaye 2002 hadi 2003 nikasoma cheti cha elimu maalumu katika Chuo cha Patandi.
Mwaka 2005 hadi 2007 nikasomea stashahada ya elimu ya watu wazima na maendeleo ya jamii, taasisi ya elimu ya watu wazima. Mwaka 2008 hadi 2011 nikasomea Shahada ya Sayansi ya Siasa MNMA. Pia nimefundisha shule mbalimbali kwa zaidi ya miaka 15, vilevile ninajishughulisha na ujasiriamali.
SWALI: Unauzungumziaje mchakato wa Uchaguzi Mkuu kwa upande wako?
JIBU: Kwa ujumla mchakato ulikuwa mzuri hasa kwa vijana waliopitia upinzani ilikuwa ni fursa pekee ya kupata ubunge kwani Watanzania waliamua kufanya mabadiliko na walikuwa na dhamira ya dhati ya kuiondoa CCM madarakani. Katika jimbo langu hakukuwa na mpinzani, hii ilitokana na maandalizi ya muda mrefu niliyoyafanya. Nilijiandaa kwa miaka mitano kulitafuta jimbo na kazi kubwa niliyoifanya ya kuijenga chama kwa kufungua matawi mengi zaidi. Kipimo cha ushindi wangu nilianza kuona kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo katika vijiji 54 vya Jimbo la Kilwa Kaskazini kwenye uchaguzi wa mwaka 2009 vyama viwili tu vilishiriki ambapo CCM ilipata viti 47 na CUF viti saba. Uchaguzi wa mwaka 2014 kulikuwa na mabadiliko makubwa, CCM ilipata viti 33 na CUF viti 21. Hii ilinijengea nguvu na tumaini la ushindi katika Uchaguzi Mkuu.
SWALI: Ni changamoto gani kubwa uliyokumbananayo katika Uchaguzi Mkuu?
JIBU: Changamoto kubwa ni ukubwa wa jimbo, jimbo langu lina Kata 13 lakini eneo la Kijiografia ni kubwa sana mfano ukitoka Maredego kwenda Zinga Kibaoni ni zaidi ya km 170. Mtazamo wa wapiga kura ni kwamba wao wanadhani kwamba wagombea wana fedha jambo ambalo si la kweli. Pia changamoto nyingine ilikuwa wagombea wa CCM kulindwa na vyombo vya dola, mfano katika jimbo langu mpinzani wangu Mangungu alitoa gari tatu za wagonjwa bila ya kufuatiliwa na Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru).
SWALI: Unadhani Ukawa umechangia vipi katika ushindi wako na kunyakua Jimbo la Kilwa Kaskazini?
JIBU: Ukawa ulikuwa injini ya ushindi wangu. Kupitia Ukawa watanzania wote walijiona wamoja na jukumu lao kubwa ilikuwa ni kuiondoa CCM madarakani, hilo lilinibeba sana.
SWALI: Nini mikakati yako kwa wapiga kura wako?
JIBU: Mikakati yangu kwa wapiga kura ni kuwaletea maendeleo. Katika nyanja za kilimo nitaweka msisitizo kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula ili wananchi wasikumbwe na njaa. Pia nimepeleka elimu mpya ya uzalishaji wa zao la alizeti ambalo kwa utafiti nilioufanya linastawi vizuri jimboni kwangu. Kwa upande wa maji ninaishawishi Serikali na wadau wengine kuondoa tatizo la maji kwa kuchimba visima virefu na vifupi katika vijiji jimboni. Katika kata ambazo zinapakana na bahari ya Hindi ninafanya ushawishi kwa serikali kuleta mitambo ya kubadilisha maji ya bahari na kuyaondoa ya chumvi ili yatumike kwa matumizi ya kawaida.
Kuhusu elimu, naendelea kufanya ushawishi kwa kushirikiana na baraza la Halmashauri kuasisi mfuko wa elimu ambao utachangiwa na pato la ndani la Halmashauri ili kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo sitofahamu ya elimu bure. Pia nitashawishi kuanzishwa shule ya kidato cha tano na sita katika jimbo langu.
Vile vile nitaisimamia Serikali kupanua Bandari ya Kilwa Masoko ili kuwezesha meli kubwa kutia nanga katika bandari hii. Kwa upanuzi huu itasaidia kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa kuja Kilwa . Kwa mfano tuna changamoto kubwa ya bei ya ufuta zao ambalo linazalishwa kwa wingi katika wilaya yetu, tukiwa na bandari yenye uwezo mkubwa wafanyabiashara wakubwa watakuja kununua ufuta bandari ya Kilwa badala ya Dar es Salaam, hivyo kuwezesha bei ya ufuta kupanda kwa mkulima.
SWALI: Ni kero gani sugu iliyopo katika jimbo lako?
JIBU: Kero sugu iliyopo jimboni kwangu ni ukosefu wa maji safi na salama na bado vijiji vingi havina maji.
SWALI: Umejipanga vipi kumaliza kero hiyo ya maji?
JIBU: Ili kumaliza kero ya maji katika jimbo langu, nimejipanga kusimamia serikali kujenga mradi mkubwa wa maji kutoka chanzo cha mto Rufiji na tayari nimeuliza swali bungeni na serikali imekubali kwanza kufanya utafiti wa namna gani wataanzisha mradi huo.
SWALI: Wewe ni Mwenyekiti wa LAAC, unadhani kitu gani kilikushawishi ukagombea nafasi hiyo?
JIBU: Kilichonishawishi ni dhamira yangu ya dhati ya kutaka kusimamia matumizi ya fedha za wananchi katika maeneo yao.
SWALI: Je, kuna changamoto gani iliyopo katika kamati yako?
JIBU: Changamoto kubwa mpaka sasa iliyopo katika kamati yangu ni kushindwa kuzifikia Halmashauri nyingi mpaka sasa tumekagua Halmashauri 30 kati ya 163. Nikiwa kama kiongozi wa kamati ya LAAC, tumejipanga kukagua halmashauri nyingi kadiri iwezekanavyo.
SWALI: Kwanini mmeshindwa kuzifikia Halmashauri nyingi?
JIBU: Kwa ujumla kikwazo kikubwa ambayo imesababisha tushindwe kuzifikia Halmashauri nyingi ni kwa kuwa Bunge ni jipya, hivyo uundwaji wa kamati ulichelewa.
SWALI: Je, wabunge wa CCM wanakupa ushirikiano katika kamati yako?
JIBU: Wabunge wote wananipa ushirikiano wa kutosha tukiwa kwenye Kamati chini ya uongozi wangu kinachotangulia ni wajibu na majukumu ya Kamati, kwa hiyo suala la uchama hakuna.
SWALI: Unauzungumziaje mwenendo wa Bunge?
JIBU: Mwenendo wa Bunge hauendani na aina ya wabunge waliopo. Bunge limekuwa ni taasisi isiojiamini. Bunge limeshindwa kupambana na changamoto za wabunge vijana wenye ari ya kuwatumikia wananchi. Shughuli za Bunge zimekuwa za sirisiri, Bunge sasa si darasa la kuwafundisha Watanzania bali ni jando la kuwafunda wabunge waendane na serikali inavyotaka.
SWALI: Wabunge wa upinzani mmemsusia Naibu Spika, pengine unadhani anakosea wapi?
JIBU: Kosa lake ameshindwa kutumia vizuri ualimu wake, ameshindwa kulisoma Bunge na aina ya wabunge waliopo alitakiwa awatibu kisaikolojia (sociological treatment)
Si sahihi kufikiri kwamba kila kinachofanywa na upinzani ni kibaya.
SWALI: Pengine sasa nini ushauri wako kwa kiti cha Spika?
JIBU: Ushauri wangu kwa kiti cha Spika hasa Naibu Spika anatakiwa asiegemee upande mmoja katika kufanya uamuzi asikilize wapinzani kwa sababu nao wana mambo mazuri kuliko wale wa CCM. Mwisho.