NA MANENO SELANYIKA, DAR ES SALAAM
MADEREVA 16 wa pikipiki, magari na bajaji wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo kuendesha vyombo vya moto katika barabara ya mabasi ya mwendo wa haraka (DART).
Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya mahakimu tofauti katika mahakama hiyo huku wengine wakikosa dhamana hivyo kuendelea kusota mahabusu.
Waliopandishwa kizimbani ni Joseph Shirinde (29), Abdulkarim Adam (34), Hussein Kadima (38), Bahati William (18), Hassan Mohamed (30), Nasri Salum (23), Florens Valerian (32), Rashid Sheha (45), Safiel Msofe (32), Matatizo Matonya (23), Jeremiah Amos (25).
Wengine ni Haji Ramadhan (25), Peter James (30), Rashid Kassim (24), Ally Ramadhan (22) na Mohamed Issa (23).
Mbele ya Hakimu Mfawidhi, Said Ding’ohi, Wakili wa Serikali Grace Lwila alidai watuhumiwa walifanya makosa hayo Juni 3 mwaka huu katika maeneo mbalimbali kwenye barabara ya Morogoro.
“Watuhumiwa Shirinde, William na Ramadhani mnadaiwa kuendesha vyombo vya moto kwenye barabara ya mabasi ya mwendokasi huku mkitambua kuwa ni kinyume cha taratibu na sheria za usalama barabarani,” alidai Wakili Lwila.
Lwila alidai makosa mengine yanayowakabili watuhumiwa hao ni kuendesha gari, pikipiki na bajaji katika barabara ya umma bila kuwa na leseni wala bima.
Hakimu Ding’ohi alisema kwamba kwa mujibu wa sheria kila mshtakiwa anatakiwa awe na mdhamini mmoja aliyeajiriwa katika taasisi yoyote inayotambulika kisheria atakayeweka saini ya maandishi ya Sh 200,000 kwa kila mmoja.
Washtakiwa wengine 13 waliobakia walifikishwa mbele ya Hakimu Obadia Bwegego, Hanifa Mwingira na Hakimu Boniface Lihamuke wakikabiliwa na mashtaka ya kutumia barabara hiyo ya mabasi ya mwendo wa haraka. Washtakiwa wote walikana mashtaka isipokuwa Shirinde ambaye alikiri tuhuma.
Hakimu Saidi alimtaka mshtakiwa huyo kulipa faini ya Sh 110,000 au kwenda jela kwa kila kosa mwaka mmoja kwa makosa matatu. Hata hivyo hakuweza kulipa faini hiyo.
Kesi hizo zimeahirishwa hadi Juni 20 mwaka huu, Abdulkarim Adam na Hussein Kidima waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana wakati wengine walirejeshwa mahabusu hadi watakapokamilisha masharti hayo.