26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mume ashikiliwa mauaji ya dada wa bilionea Msuya

dada wa bilionea Erasto MsuyaNa Asifiwe George, Dar es Salaam

SIKU chache baada ya dada wa bilionea Erasto Msuya kuuawa kwa kuchinjwa nyumbani kwake Kibada Kigamboni, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema linamshikilia mume wa marehemu kwa tuhuma za kuhusika na kifo hicho.

Mbali na hilo, pia jeshi hilo linamsaka mfanyakazi wa ndani wa marehemu Anathe Msuya ambaye anadaiwa kuondoka siku moja kabla ya kutokea kwa mauji hayo ya kinyama.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema wamelazimika kuunda jopo linaloshirikisha vigogo watano wa jeshi hilo ambao ni wataalamu wa upelelezi ili kubaini kwa undani mauaji hayo ya kutisha.

Pamoja na hali hiyo, imebainika katika uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi, mume wa marehemu Anethe anahusishwa na mauaji hayo ambapo inadaiwa kuwa alikwenda nyumbani kwa marehemu akiwa na pikipiki siku ya tukio hilo.

“Mtuhumiwa huyo tunaendelea kumshikilia kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili tuweze kubaini mtandao mzima uliohusika katika tukio hilo.

“Niwahakikishie kwamba watu waliotekeleza mauaji hayo tutawakamata tu, na watakuwa mfano kwa wengine, kama mtu amegombana na mwenzake hakuna haja ya kumuua, wanawake na wanaume wamejaa kibao unaweza ukatafuta mwingine ukaoa au ukaolewa na si kufanya mauaji ya kinyama kiasi hicho,” alisema Kamanda Sirro.

Kutokana na hali hiyo kamanda huyo wa polisi aliwataka wananchi kuwa na subira ili kuwapa nafasi ya kufuatilia tukio zima.

Kifo cha Anethe kilitokea Mei 26 mwaka huu katika eneo la Kibada blok 16 Kigamboni akidaiwa kuchinjwa na watu wasiofahamika.

Taarifa za ndani ambazo gazeti hili lilizipata toka Mbezi Makonde uliko msiba wa Anethe, zinaeleza kuwa matukio yanayofanana na hayo yamekuwa yakiiandama familia hiyo tangu kaka yao Erasto auawe mwaka 2013.

Mmoja wa wanafamilia hiyo alisema baada ya Erasto kupigwa risasi, dada yao aliyetajwa kwa jina la Antuja naye alimwagiwa kitu kinachohisiwa kuwa ni sumu wakati akiwa amelala chumbani na hivyo kumuathiri.

Wakati akimwagiwa sumu hiyo, inaelezwa kuwa Antuja ambaye ni mfanyabiashara wa maduka ya nguo, alikuwa amelala pamoja na mtoto wa marehemu Anethe aitwae Allan.

Tukio jingine ni lile lililotokea Desemba mwaka jana ambapo dada yake aitwae Ester na muwewe walipigwa risasi za mgongoni na kifuani wakiwa katika baa ya Hongera iliyopo Bamaga Sinza, Dar es Salaam.

Kutokana na matukio hayo kuiandama familia yao, baadhi ya ndugu wamesema yanatokana na visasi ambavyo wanasema kuisha kwake kutatokana na Rais John Magufuli kuingilia kati.

Kuhusu maisha ya kimapenzi ya marehemu Anethe, ndugu huyo alisema hayakuwa mazuri.

Alisema Anethe aliolewa na kwa bahati mbaya ndoa yake ilikaa mwaka mmoja ikaingia migogoro na hivyo kuachana na baba watoto wake.

Majirani wa marehemu Anethe walikataa kuzungumza chochote juu ya tukio hilo wakisema hakuna wanalolifahamu zaidi ya kuona askari wakiwa na gari waliofika nyumbani hapo juzi  na kisha kuuchukua mwili na kuondoka nao.

Taarifa nyingine zinaeleza kwamba Anethe alikuwa mstari wa mbele katika kesi ya mauaji ya kaka yake bilionea Erasto Msuya ambayo inaendelea kusikilizwa hadi sasa Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Kaka yake huyo aliuawa kwa kumiminiwa risasi 22 Agosti 7, 2013 katika Uwanja wa ndege wa KIA na hadi sasa watu saba wanashikiliwa kwa kosa hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles