MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope ameahidi kumpa zawadi ya gari beki wa kulia wa timu hiyo, Mohammed Hussein `Tshabalala` kutokana na nidhamu ya hali ya juu aliyoionesha ndani ya kikosi cha Simba.
Tshabalala aliyesajiliwa na klabu hiyo misimu miwili iliyopita akitokea Kagera Sugar, ameonyesha kiwango kilichomfanya aaminiwe na kila kocha aliyeifundisha klabu hiyo katika muda wote alioitumikia Simba na kuwa miongoni mwa wachezaji wasiokosekana kwenye kikosi cha kwanza.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Hanspope alisema ni kweli alitoa ahadi ya gari kwa mchezaji huyo Novemba mwaka jana, kutokana na nidhamu aliyonayo ndani na nje ya uwanja.
Alisema katika kikosi cha Simba, pia kuna wachezaji ambao wameonyesha nidhamu lakini ameshawishika zaidi na Tshabalala na atafanya kama alivyomuahidi.
“Ni kweli hilo suala lipo, ahadi niliyoitoa mwaka jana kutokana na jinsi alivyoonyesha kiwango kizuri pamoja na nidhamu yake, hivyo mpango huo upo palepale,” alisema.
Alisema ni mapema kutaja aina ya gari atakalompa beki huyo, hadi mipango hiyo itakapokamilika ndipo wataliweka wazi.
Wakati huo huo, Tshabalala alisema anafurahi kuona mchango wake katika timu unathaminiwa na kila mmoja na juhudi zake binafsi, zimemsababisha kiongozi huyo kuamua kuahidi kumpa zawadi hiyo.
“Hilo jambo kwangu ni jipya, ila nafurahi kusikia hivyo na nina imani kwamba mchango wangu unathaminika kwa viongozi, mashabiki na wanachama,” alisema.
Tshabalala alisema licha ya ahadi hiyo pia anawashukuru mashabiki kwa kumpa zawadi ya viatu, anawahakikishia ataendelea kujituma na kujitolea kurejesha heshima kataka timu yake.