MBUNGE wa Chambani, Yusuph Salum Hussein (CUF) jana alichafua hali ya hewa bungeni baada ya kusema kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilitumika kupindua Mapinduzi ya Zanzibar katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu visiwani humo.
Alikuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Wakati akichangia bajeti hiyo, Yusuph alisema jeshi limekuwa likifanya kazi katika mazingira magumu lakini limetumika kupindua Mapinduzi ya Zanzibar na limetengewa asilimia 18 katika bajeti ya maendeleo.
Wakati anaendelea kuzunguma Spika wa Bunge, Job Ndugai alimwambia:” Mheshimiwa Yusuph umetumia maneno ambayo yanatupa tabu, kwamba jeshi limetumika kupindua Zanzibar…hebu liweke vizuri.”
Baada ya kauli hiyo ya Spika, Yusuph alijibu akisema:”Mheshimiwa Spika Oktoba 25 mwaka jana kulikuwa kuna Uchaguzi Mkuu, wananchi wa Zanzibar wakachagua chama chetu cha CUF lakini baadaye uamuzi ule ukapinduliwa…naendelea ambaye hajaridhika anione nimsomeshe,”alisema huku wabunge wa CCM wakizomea.
Alipomaliza kuchangia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister Muhagama aliomba mwongozo kwa Spika akitumia kanuni 68 (7)
“Maana ya mapinduzi wote tunafahamu na hasa katika uchaguzi, leo tunapotoa taarifa kwamba jeshi ambalo hata mbunge anayechangia amelisifia …anapokuja kulituhumu kwamba limefanya mapinduzi ni jambo ambalo si kweli kabisa”.
Hapo Spika Ndugai alisimama akimwambia Yusuph kwamba amesikia maelezo ya waziri hivyo afute kauli yake.
“Mheshimiwa Spika sifuti kauli yangu kwa sababu ninao ushahidi wa kila kituo kwamba chama chetu kilishinda na ninachokisema ninakiamini ndani ya nafsi yangu,”alisema huku Spika akimwambia anampa nafasi ya mwisho kufuta kauli hiyo na kwamba asilete habari ya vyama.
Hatimaye Yusuph alikubali kufuta kauli yake huku Spika akiwataka watu wa hansard kufuta kauli hiyo ya jeshi kupindua Zanzibar na lisionekane mahali popote.
Mdee ahoji kiinua mgongo cha wanajeshi
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) alihoji kiinua mgongo cha wanajeshi waliopigana vita ya Uganda mwaka 1978/79 ambako nchi hiyo ililipa Sh bilioni 59.
“Nikuombe waziri hawa wastaafu tuwaangalie kwa jicho pana. Mwaka 2009 lilijibiwa swali hapa bungeni, tunakumbuka kuna wanajeshi wetu wastaafu mwaka 1978 walishiriki kwenye vita huko Uganda, Serikali ya Uganda ikatoa kiinua mgongo cha Sh bilioni 59.
“Mkajibu kwamba hizo fedha mtawapa miaka saba baadaye mkachikichia na mkwanja wa watu. Hiki kifuta jacho cha wanajeshi wetu waliopambana usiku na mchana kuokoa nchi yetu kipo wapi?
“Naomba utuambie leo usije ukasema oh muda hautoshi. Tunataka majibu kwa sababu wanajeshi wastaafu wanataka kujua hizo fedha zimekwenda wapi,”alisema Mdee.