27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Sukari ya serikali yatua nchini

Kassim MajaliwaNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali imeagiza tani 70,000 za sukari kutoka nje ya nchi ili kukabiliana na uhaba uliopo.

Amesema kati ya hizo, tayari tani 11,957 zimewasili nchini na zitaanza kusambazwa kesho.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam jana, Majaliwa alisema sukari ambayo imewasili nchini, itasambazwa kwa utaratibu maalumu.

Alisema tani 2,000 zitapelekwa mikoa ya kaskazini, tani 3,000 Kanda ya Ziwa, tani 2,000 mikoa ya kusini, tani 2,000 Nyanda za Juu Kusini na tani 2,000 Kanda ya Kati.

“Tani nyingine 24,000 za sukari zitawasili Ijumaa hii na hadi zitoke bandarini, itakuwa kama Jumapili… kwa hiyo zinaweza kusambazwa kuanzia Jumatatu. Tani nyingine 20,000 zitawasili baadaye, ama mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwanzoni mwa Juni,” alisema Majaliwa.

Aliwataka Watanzania wasihofu kuhusu uhaba wa sukari uliojitokeza hivi karibuni, kwani umesababishwa na watu wachache.

“Mheshimiwa Rais ameagiza watu waliohodhi bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe. Lakini tunaagiza kwa muda mfupi kwa sababu viwanda vyetu vinatarajia kuanza uzalishaji ifikapo Julai,” alisema.

Amewataka wasambazaji wa sukari waiuze kwa wafanyabiashara wadogo ili wao wawauzie wananchi kwa bei elekezi ya Sh 1,800.

Pia amewaagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha wanasimamia ukaguzi wa sukari ili kubaini zaidi wale waliohodhi bidhaa hiyo.

Alisema mkakati wa Serikali ni kuongeza uzalishaji wa sukari na nia ni kuhakikisha tatizo la uhaba uliopo linakwisha ifikapo 2019.

“Wananchi wasiogope, Serikali imechukua hatua kwa udhibiti mzuri ili tusije kuporomosha soko letu la ndani.

“Tunao mkakati wa kuboresha viwanda vya ndani, wenye viwanda wenyewe au kwa ubia na wawekezaji kutoka nje, wanaweza kufungua mashamba kwenye maeneo matatu tuliyotenga kwa ajili hiyo.

“Serikali imetenga maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa ambayo ni Bagamoyo, Ngerengere na Kigoma. Huko wanaweza kulima na kujenga viwanda vya sukari na uzalishaji ukawa unapanda mwaka kwa mwaka hadi tutakapomaliza tatizo hili,” alisema.

Rais John Magufuli aliagiza vyombo vya dola kuwakamata wafanyabiashara wote ambao wameficha sukari katika maghala yao.

Agizo hilo limesababisha tani nyingi za sukari kukamatwa maeneo mbalimbali nchini, huku kiasi kadhaa kikitaifishwa na kugawiwa wananchi.

Juzi akiwa mkoani Arusha, Rais Magufuli alisema hakuna mfanyabiashara atakayepona, awe ni mwana CCM, Chadema au CUF, kwake ni mkong’oto tu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles