29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Kamishna Nzowa: Ningekuwa IGP ningefumua Jeshi la Polisi

KKELIYA MBONEA NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA

ALIYEKUWA Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishina Mstaafu Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, Godfrey Nzowa, amesema kuna baadhi ya viongozi nchini hawana dhamira ya kweli ya kukomesha biashara ya dawa za kulevya.

Amesema kukosekana kwa dhamira ya kupambana na tatizo hilo, ni hatari zaidi kwa Tanzania kufanywa soko la kudumu la kuuzia na kuendelea kuwa kituo cha kupitisha dawa hizo kama inavyofanyika sasa.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu mkoani hapa, Nzowa aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, alisema ili kufanikisha vita hiyo, kunahitajika watumishi wa umma wenye moyo wa uzalendo na kujitolea kwa nchi yao.

Kamishna huyo mstaafu ambaye ni miongoni mwa maofisa wa polisi walioacha rekodi iliyotukuka ya utendaji kazi, alisema tofauti na zamani, vijana waliochaguliwa kujiunga na jeshi hilo, walipitia mchujo mkali na hivyo kuwa watumishi wenye nidhamu.

“Hakuna uangalizi (super vision), siku hizi viongozi hawalipendi wala kulithamini Jeshi la Polisi, kama wangelipenda, vijana wanaojiunga wangechujwa vyema tangu malezi, wale wenye karama walizozaliwa nazo, na hata kuhojiwa ana kwa ana kama zamani.

“Nikiingia leo, na kama ningekuwa IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi) ningewatumbua wote, askari wengi hawana wito, zamani sisi hatulali, ‘morning call’ ilikuwa saa 12:00, sasa hivi hakuna,” alisema Nzowa.

Aliwaonya baadhi ya viongozi wa Serikali wanaodhani njia pekee ya kutokomeza usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, inahitajika silaha za kisasa, mbwa na mashine za utambuzi.

Alisema wafanyabiashara wa dawa za kulevya ni watu wasomi, wabunifu na wajanja wenye kasi ya kubadilisha na kubuni mbinu za kisasa kila siku ili tu kukabiliana na vyombo vya dola.

Alizitaja baadhi ya mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji hao wa dawa za kulevya, kuwa ni pamoja kututumia wajawazito ambao ni vigumu kuhisi au kuwatilia shaka kama wamemeza dawa hizo.

“Baada ya mbinu za kutumia maiti kugundulika, sasa wajawazito, si rahisi kama si mdadisi kumshuku mjamzito… hawa watu wanaweza kupita mbele yako. Kunahitajika roho ya kizalendo, ujasiri na kujitolea ili kumkagua mama mwenye mimba,” alisema Nzowa.

Aliyataja maeneo ya viwanja vya ndege kuwa yapo kwenye changamoto kubwa za ukaguzi na ukamataji ambapo wasafirishaji wa dawa hizo za kulevya, wamekuwa wakificha hata sehemu ambazo mtu huwezi kutegemea.

Alisema bila ya dhamira ya kweli, kwa watu waliopewa dhamana kutimiza wajibu wao hakuna kinachoweza kukamatwa.

Nzowa alisema viwanja vingi vya ndege, kikiwamo cha Julius Nyerere cha Dar es Salaam, kumekuwapo na mbinu za kisasa zinazofanywa na watu hao ili mradi tu waweze kupita bila kugundulika.

“Kuna wakati nilipata wakati mgumu sana kuwakamata watu waliokuwa na hati za kusafiria za kidiplomasia (mabalozi), hawa walikuwa ni mabalozi bandia na walikuwa wamebeba dawa za kulevya. Unaanza kuwakamata watu kama hao wenye kinga kwa mujibu wa Azimio la Viena.

“Watu hawa walikuwa makini, wenye mwonekano maridadi, wanaojua kusoma jiografia ya dunia na kuyajua maazimio mbalimbali ya Umoja wa Mataifa juu ya viongozi wenye hadhi ya kidiplomasia duniani wanatakiwa kupewa heshima ipi.

“Kama huna dhamira ya dhati na taarifa sahihi kwenye kazi hii, watu makini kama wale huwasimamishi, huwakagui wala huwabaini wanapopita uwanja wa ndege.

“Tulifanikiwa kuwakamata na kuwakagua na tulipoanza tu, mmoja alivua koti akatupa kule na jasho kuanza kumtoka,” alisema.

Alisema mtu huyo alikuwa na nyaraka zote zinazoonyesha ni mwanadiplomasia mwenye kinga ya kutokaguliwa.

 

RAIA WA UGANDA

Alisema changamoto nyingine aliyoipata akiwa kazini, ni tukio la raia wawili wa Uganda waliojitambulisha kuwa maofisa kutoka Ikulu ya nchi hiyo, waliokuwa wakisafirisha dawa kutoka Peru kupitia Malawi na Tanzania.

“Kama nilivyosema, hawa ni wajanja na wabunifu, nilipopata taarifa kwa msiri wangu, niliweka vijana wangu tayari… kwa kawaida huwa sijionyeshi kwao kwa sababu za kitaaluma. Bahati mbaya walipokamatwa na kuhojiwa walijieleza wanatokea Ofisi ya Rais Uganda.

“Na walionyesha mabegi yenye nembo ya nchi, hati ya kusafiria yenye hadhi ya kidiplomasia na vitambulisho ambavyo havikuwa halisi. Kwa bahati mbaya wakubwa walikubali waachiwe.

“Lakini kibaya zaidi, walipelekwa hoteli yenye hadhi ya nyota nne kisha wakalipiwa gharama zote wakidhani ni maofisa kweli, kumbe hakuna kitu,” alisema Nzowa.

Alizataja mbinu nyingine kuwa wasafirishaji wanapenda kutumia nguo za mitumba, hasa mataulo, ambayo huyalowanisha maji kisha kuchanganya na dawa za kulevya kabla ya kufungwa.

Alisema pindi mzigo unapofika sehemu husika, taulo hizo huanikwa juani kisha dawa kujitenga.

 

NINI KIFANYIKE

Alisema ili kufanikiwa kupiga vita usafirishaji na matumizi ya dawa hizo, ipo haja kubwa ya kuendelea kubadilishana taarifa na kufanya misako ya pamoja kuanzia ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.

“Tatizo lililopo ni kwamba wahusika wa usafirishaji dawa za kulevya hawana mipaka, wanapita mahali popote unapoweza kupajua wewe. Hadi sasa hakuna nchi ambayo haijaathirika na tatizo hili, tunahitaji kushirikiana kwa kubadilishana taarifa, hilo ndilo la msingi,” alisema Nzowa.

 

MAISHA

Akisimulia kwa ufupi maisha yake, baada ya kustaafu, Kamishina Nzowa alisema kila mara amekuwa akipokea ujumbe wa vitisho.

“Usalama wangu unategemea Mungu zaidi, kama mnavyojua, ukistaafu hakuna mwenye habari na wewe,” alisema Nzowa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles