30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Hukumu yawatia kiwewe wabunge EALA

Makongoro Nyerere
Makongoro Nyerere

NA PATRICIA KIMELEMETA, DAR

SIKU chache baada ya Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kutoa hukumu ya kukiukwa kwa Ibara ya 50 ya mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wabunge wa Tanzania wanaoshiriki katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wanakusudia kukutana ili kujadili kwa kina hukumu hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere alisema kati ya wabunge hao kuna wanasheria watatu ambao watatoa mwongozo wa nini kifanyike ili kuchukua uamuzi unaofuata ikiwa ni pamoja na kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Alisema wabunge hao watakutana wakati wowote kuanzia sasa na kuangalia namna ambavyo wanaweza kukabiliana na hukumu hiyo.

“Unajua hukumu imetoka wakati wengine hatupo nchini lakini tumesikia…tumewasiliana…na tumepanga kukutana ili kuijadili kisheria zaidi jambo ambalo linaweza kutusaidia kama tutaamua kukata rufaa au la.

“Tuna wanasheria watatu, hao wataweza kutupa mwongozo wa nini tufanye ili kuhakikisha kuwa tunapinga hukumu hiyo katika kipindi hiki ambacho hukumu hiyo imetolewa,” alisema Makongoro.

Aliongeza jaji aliyetoa hukumu hiyo hakuangalia mkataba wa Afrika Mashariki na mgawanyo wake wa uwakilishi katika ubunge, kwa sababu hakuna kipengele kinachoonyesha kuwa lazima kambi rasmi iwe na mwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki.

Alisema hivi karibuni marais wa Afrika Mashariki akiwamo, Uhuru Kenyatta na Yoweri Museven walisaini mkataba uliounda upya jumuiya hiyo ambao unatoa uwakilishi wa ubunge.

Mbunge huyo alisema mkataba huo unaeleza chama kinachotawala kinatoa idadi kubwa ya wabunge katika uwakilishi huo na idadi iliyobaki inatoka katika chama chochote cha upinzani na si lazima chama hicho kiwe kambi rasmi ya upinzani bungeni.

“Kwa mfano…, kama asilimia 80 wanatoka chama tawala, asilimia 20 wanapaswa kutoka chama chochote cha upinzani, mkataba hausemi lazima atoke kambi rasmi ya upinzani bungeni,” alisema.

Alisema katika uteuzi wake, Spika Anne Makinda alitoa nafasi mbili kutoka upinzani, nafasi mbili kutoka Zanzibar na nafasi tano kutoka bara.

Katika hukumu yake iliyotolewa mwishoni mwa wiki, Mahakama ya Afrika Mashariki ilisema Bunge la Tanzania lilikiuka ibara ya 50 ya mkataba wa kuanzishwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Jaji Kiongozi, Jean Bosco-Butasi akiwa na majaji wengine wa mahakama hiyo, Isaac Lenaola na Jaji Faustine Ntezilyayo, walitoa uamuzi huo katika kesi iliyofunguliwa na Antony Komu, aliyekuwa mgombea ubunge wa EALA kupitia Chadema.

Hukumu hiyo iliyokuwa na kurasa 38, mahakama hiyo ilimpa ushindi Komu katika hoja zake zote tatu na kutupilia mbali pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kesi hiyo na hivyo kuitaka Serikali kulipa gharama za kesi hiyo.

Katika madai yake ya msingi, Komu alikuwa anapinga utaratibu uliotumika kupata wagombea wa Bunge la EALA kutoka Tanzania, akidai ulikiuka Ibara ya 50 ya mkataba wa kuanzishwa kwa EAC inayoelekeza wabunge wapatikane kwa kuzingatia uwiano na makundi.

Ibara hiyo inaeleza kuwa, Bunge la Taifa kutoka kila nchi mwanachama litachagua wabunge tisa kutoka nje ya wabunge wa bunge husika kuwa wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzingatia uwiano wa vyama vya siasa, jinsia na makundi mengine.

Komu pia alikuwa akitaka tafsiri ya kisheria iwapo Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda kupitisha jina la mgombea wa Chama cha TADEA, John Lifa Chipaka, hali ya kuwa chama chake hakina mwakilishi bungeni.

Pia alitaka kujua kama ni halali kwa chama kikuu cha upinzani nchini, kinachounda baraza kivuli la mawaziri, kukosa uwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki.

Katika uamuzi wa majaji wa mahakama hiyo, wameamua kuwa uchaguzi huo ulikiuka ibara ya 50 ya kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na upatikanaji wa wabunge wa Bunge hilo.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Tunaona tofauti kati ya mahakama za Tzna mahakama za kikanda za Afrika mashariki,hapa Tz mahakama hazitoi haki, bali zinahukumu kesikutokanana kutazama ni nani anadaiwa, na pengine kutokana na rushwa mahakamani basi hasi inawawa. Hili ni fundisho kwa mahakama nchini Tanzania kuzingati haki na mfumo wa sheria husika. Ni lini mahakama zet zitaanza kutoa haki kwa walengwa? KIla wakati ni kukata rufaa, kata rufaa, hii ni nini? Nchi nainwekdan wapi? Kweli nchi inahitaji katiba mpya iliyobora na pia serikali mpya yenye upeo wa kufikiri. Lakini serikali hii ya CM ambayo imemechoka ile mbaya pamoja na kukosa mwelekeo kabisa. Kilichobaki ni propaganda (porojo), kejeli, na kutumia vyomo vya dola (polisi, usalama wa taifa, jeshi na mahakama). nchi ya taifa imegeuka ya kipolisi, hata Tibaigana amesema polisi acheni kukandamiza hovyo waandamanaji na kuwajeruhi. Hii ina maana sasa Tz imekuwa nchi ya Kipolisi, utawala kwa nguvu ya polisi ndivyo inavyoonekana sasa katika picha huku nje ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles