Na Waandishi Wetu
KWA nyakati tofauti; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Jeshi la Polisi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kwa kauli na vitendo vyao, bila kujua wamejikuta wanamweka pabaya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili juzi na jana umebaini kuwa mitaani watu wanasema wazi kuwa kupigwa ovyo kwa watu na askari polisi, wakiwamo waandishi wa habari, katika siku za hivi karibuni kuna baraka za Serikali.
Kwamba hii inatokana na kauli iliyotolewa bungeni mapema mwaka huu bungeni mjini Dodoma na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliposisitiza kuwa wananchi wasiotii amri halali za Serikali lazima wapigwe tu.
Aidha, tukio la waandishi wa habari kupigwa na askari polisi Alhamisi ya wiki hii wakitekeleza majukumu yao wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipofika Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam kuhojiwa kuhusu tuhuma za uchochezi, limehusishwa moja kwa moja na kauli ya Waziri Mkuu Pinda.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, tayari amelaani kitendo cha kupiga waandishi wa habari kwamba ni cha kinyama na ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akihutubia mikutano ya hadhara iliyofanyika katika Kata ya Kibiti, na baadaye katika Kata ya Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani, Profesa Lipumba alisema Katiba ya Tanzania, Ibara ya 18, inaeleza wazi kuwa wananchi wanayo haki ya kupewa taarifa zinazohusu maisha yao na Taifa kwa ujumla.
“Waandishi wa habari walitakiwa kupewa mazingira mazuri ya kupata habari kuhusu kile walichokifuata na si kunyanyaswa kama ilivyofanyika,” alisisitiza Profesa Lipumba, na kuongeza.
“Wanasema Mbowe katoa kauli za uchochezi kwenye hotuba yake, kwanini wasimshikilie pia Waziri Mkuu Pinda alipotoa maneno ya uchochezi bungeni?”
Alisema maandanao ni haki ya kisiasa hapa nchini, na kazi ya polisi ni kuhakikisha yanakuwa ya utulivu na si kuyazuia. “Kiongozi wa kambi ya Upinzani ni sawa na waziri mkuu, hivyo lazima aheshimiwe na asipotezewe muda wake ovyo,” alisema Profesa Lipumba.
Gazeti hili lilizungumza na mmoja wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, ambaye pia ni waziri mwandamizi katika Serikali ya Rais Kikwete (hakutaka jina lake litajwe), na kusema kuwa baadhi ya matukio ya kisiasa yanayotokea hivi sasa nchini yanamweka pabaya Rais Jakaya Kikwete wakati huu muda wa kumaliza kipindi chake unapoyoyoma.
Alisema kuna baadhi ya wanasiasa ndani ya chama chake wanaotaka kumkosanisha na wananchi kwa kuchagiza vifanyike vitendo fulani fulani kwa maslahi yao, vitendo ambavyo vinawaudhi wananchi.
Profesa Lipumba, kwa mujibu wa gazeti la Majira toleo la jana, naye ameliongelea suala hili tete na kumshauri Rais Kikwete awe na hadhari kuhusu hili.
“Rais Kikwete amalize muda wake vizuri pasipo kukosana na wananchi kama hali inavyojionyesha kwa sasa, kwani kuna makundi ndani ya CCM hayamtakii mema.
“…awe makini na haya makundi yanayomkosanisha na wananchi wakati huu wa kumaliza kipindi chake cha mwisho,” alisema Lipumba.
Wakati haya yakijiri, waandishi wa habari na taasisi zake wameendelea kucharuka kuhusu kupigwa kwa waandishi wa habari na askari polisi.
“Hii inaendelea kuibua hisia za chuki kwa waandishi dhidi ya Serikali, hasa tangu kuawa kwa mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daud Mwangosi, akiwa mikononi mwa polisi mkoani Iringa wakati akitekeleza majukumu yake,” amekaririwa akisema Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Kupiga Vita Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT), Edwin Soko.
Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri tayari zimekwisha kutema cheche kuhusu suala hili. Taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, miongoni mwa mambo mengine, ilisema kuwa hatua ya kuwashambulia waandishi wa habari wakati wakiwa kazini si tu inalenga kuficha ukatili uliokusudiwa kufanywa, bali inaibua chuki kati ya taasisi hiyo na vyombo vya habari bila sababu za msingi, na hasa unyasaji huo unapofanyika mbele ya viongozi wakuu wa jeshi hilo, akiwamo Kamishna wa Opesheni na Mafunzo, Paul Chagonja.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absolom Kibanda, amependekeza kuwa Jeshi la Polisi lifumuliwe kwa kuonyesha kuwa askari polisi hawajui wajibu wao.
Nalo Bunge Maalumu la Katiba ambalo linaendelea na vikao vyake bila kuwapo kwa maridhiano na Upinzani, linaonekana pia kutokuwa na mwelekeo wa kuwafurahisha Watanzania, na pengine kumgeuka mwasisi aliyeanzisha mchakato wa kutunga Katiba Mpya, Rais Kikwete.
Watu wanauliza na kushangaa ilikuwaje Rais anatoa nyongeza ya vikao hadi Oktoba 4 mwaka; huu na uongozi wa Bunge, chini ya Mwenyekiti Samuel Sitta, ukasema unaongeza hadi mwisho wa mwezi huo? Rais Kikwete anasema hivi na Sitta anasema vingine, na bado Rais anakaa kimya!
Aidha, wananchi wanakasirishwa kwa kufutwa kwa vipengele muhimu katika Rasimu ya Katiba, hali inayotishia kupatikana kwa Katiba Mpya kama ilivyokusudiwa kwa maana ya Katiba Mpya hasa, kwani Katiba itakayopatikana haitakuwa tofauti na iliyopo sasa.
Katiba Mpya si kuandika waraka mpya, ni kuhakikisha kwamba kuna tofauti kati ya Katiba hiyo na ile ya zamani kwa malengo ya kukidhi matakwa mapya ya Watanzania.
Watanzania wanamwona Sitta kuwa ndiye tatizo, wanamkasirikia, lakini pia wanamkasirikia zaidi Rais Kikwete asiyemwekea breki.
Tumuombe MUNGU atuepushe na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyo ratibiwa kisiri na viongozi walio madarakani wakijuwa kuwa wao na familia zao watakimbilia MREKANI walipojiandalia.kwani sehemu kubwa ya utajiri wa nchi yetu wamepewa watu wa marekani.