22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Kikwete: Afrika inaweza kupunguza umasikini

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

NA MWANDISHI MAALUMU, WASHINGTON

RAIS Jakaya Kikwete amesema pamoja na changamoto nyingi ambazo nchi za Afrika zinakumbana nazo, bado kuna uwezekano wa kuupunguza umasikini.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika mkutano unaojadili maendeleo na kumaliza umasikini ulioandaliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

“Tukiwa na sera sahihi, Serikali kuingilia kati pamoja na ushirikiano na sekta binafsi, inawezekana kuondoa umasikini. Juhudi hizi zikifanikiwa inawezekana kuondosha umasikini,” alisema Rais Kikwete.

Akitolea mfano wa mafanikio ambayo Tanzania imeyafikia hadi sasa katika mkutano huo, Rais Kikwete ameelezea hatua za maendeleo na kiuchumi pamoja na changamoto zake kuanzia wakati wa uhuru hadi leo.

Alisema mafanikio ya kiuchumi yameanza kuonekana nchini Tanzania baada ya kutangazwa kwa mageuzi ya uchumi katika miaka ya 1980 ambapo nchi ilidumu nayo na kuonyesha mafanikio.

“Uchumi umekua kutoka asilimia 3.5 mwaka 1990 hadi kufikia kiwango cha asilimia saba katika kipindi cha miaka 10 iliyopita,” alisema Rais Kikwete.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, bado kiwango cha kuondosha umasikini hakijaridhisha vya kutosha.

Rais Kikwete alisema kiwango hicho cha uchumi hakiridhishi kwa sababu sekta muhimu ya kilimo ambayo ndiyo inayotoa ajira kwa Watanzania wengi, haijakua na kuendelea vya kutosha na badala yake sekta zinazohusika na utoaji huduma, mawasiliano, ujenzi, uzalishaji na madini ndiyo zimekua zaidi.

“Sekta ya kilimo ambayo ndiyo inawahudumia Watanzania wapatao asilimia 75 kwa njia ya ajira na kujikimu kimaisha, imekua kwa wastani wa asilimia 4.2 katika kipindi cha miaka 10,” alisema Rais Kikwete.

Alisema tatizo hilo ndilo limefanya juhudi za kuondosha umasikini nchini Tanzania kutokufanikiwa kwa kiwango kinachotarajiwa.

Rais Kikwete yuko nchini Marekani na Jumatano ya wiki ijayo anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN).

Pamoja na kutoa hotuba hiyo, pia anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani unaotarajiwa kuwa nchi za Afrika zitatoka na msimamo wake kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi na utajadiliwa na kupelekwa katika UN katika kikao chake kikubwa kinachotarajiwa kufanyika Septemba 23.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry katika hotuba yake ya ufunguzi amemzungumzia Rais Kikwete kuwa ni kiongozi mtendaji na ambaye amechangia katika kuleta amani katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu na kukuza utawala bora nchini Tanzania.

“Maneno ya Rais Kikwete sio maneno tu, ni kiongozi anayetenda na kufanikisha mambo, tunamshukuru kwa kukuza amani katika nchi za Maziwa Makuu na utawala bora Tanzania,” alisema Kerry.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles