Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeeleza kuridhishwa kwake na hali ya usalama na afya mahali pa kazi katika kiwanda cha kutengeneza nyaya za umeme na Transfoma cha Elsewedy Electric kilichoko Kigamboni Jijini Dar es Salaam na Kiwanda cha kutengeza gypsum cha Knauf Mkuranga mkoani Pwani.
Pongezi hizo zimetolewa baada ya ziara ya kamati hiyo katika ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na viwanda hivyo, iliyofanyika Novemba 12, 2024 Dar es Salaam na Pwani.
Ziara hiyo iliongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, pamoja na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda ambapo wajumbe wa kamati hiyo walitembelea maeneo ya kazi na kujionea utekelezaji wa sheria za usalama na afya mahali pa kazi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatma Toufiq, akitoa pongezi mara baada ya kutembelea viwanda hivyo, amesema viwanda hivyo vimekuwa mfano mzuri kwa kufuata sheria na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi, akisema kamati hiyo itaendelea kutoa ushauri kwa serikali kuhusu umuhimu wa kulinda nguvu kazi ya wafanyakazi
“Tuko na wenzetu wa OSHA ambao ni miongoni mwa taasisi ambazo zipo chini ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya jamii ambapo tumetembelea maeneo mbalimbali kuangalia utekelezaji wa sheria ya usalama na afya mahali pa kazi
“Kwa taarifa tulizopata awali Knauf ni miongoni mwa kampuni ambazo zinafuata sheria na kanuni za usalama na afya mahali pa kazi vizuri na tumekuja kujionea wenyewe, sisi kama kamati tumekuwa tukiishauri serikali jinsi gani suala la usalama na afya mahali pa kazi linatakiwa liwe ili kulinda ustawi wa wafanyakazi pindi wanapokuwa kazini na tutaendelea kuishauri,” alisema Toufiq.
Awali, akizungumza mara baada ya ziara hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao ambao wanazalisha na kusafirisha bidhaa nje ya nchi, hali inayo changia kukuza uchumi wa Taifa Pamoja na kutoa fursa kwa vijana kupata ajira katika viwanda hivyo.
Sambamba na hayo, Ridhiwani aliupongeza Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara amabazo zimepelekea viwanda hivyo kuzingatia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.
“Nitumie nafasi hii kuupongeza uongozi wa OSHA chini ya Mtendaji Mkuu, Khadija Mwenda, kwenye viwanda vyote tulipo fika kabla ya kuanza kutembelea kiwanda lazima muingie kwenye chumba maalumu kupata maelekezo ya usalama na afya hususani kuhusu mambo mtakayo kutana nayo lakini pia namna ya kuweza kujilinda “ alisema Ridhiwan.
Amesema amefurahishwa namna ambavyo mifumo iliyowekwa viwandani hapo namna inavyofanya kazi na jinsi vinavyoweza kumlinda mfanyakazi.
“Nilichopenda zaidi ni namna ambavyo mifumo inavyofanya kazi viwandani hapo ukisogelea au kugusa uzio wa mashine, mitambo inazimika yenyewe jambo ambalo ni hatua kubwa sana katika kulinda usalama wa wafanya kazi, na haya yote ni matokeo ya kaguzi zinazo fanywa na OSHA mara kwa mara imepekea kufikia hatua nzuri za kiusalama maeneo hayo hali.
“Hii ni ishara nzuri ya kazi bora inayofanywa na wenzetu wa OSHA pia ni ishara nzuri kwa Mtendaji mkuu kuendelea kusimamia maagizo ya mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, sisi wasaidizi wa mheshimiwa Rais kazi yetu nikuleta ujumbe na kuhakikisha watanzania wanakua salama kama anavyotaka Rais, kwa hakika naridhishwa sana na kazi ambayo OSHA mnaifanya,” alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amewasisitiza Waajiri nchini kuendelea kuzingatia sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.
Mwenda, amesema maeneo ya kazi yanapozingatia usalama na afya kunaongeza uzalishaji kutokana na kupunguza vihatarishi kwenye maeneo yao na hivyo kuongeza uzalishaji.
“Leo tulikuwa na Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendelo ya Jamii ambayo ilikuja kuangalia jinsi ambavyo OSHA inasimamia sheria ya usalama na afya mahali pa kazi, kimsingi huu ni utekelezaji wa maelekezo tuliyo pewa tulipo kutana na Kamati ya Bunge tulitoa taarifa nzuri na kamati wakaridhishwa nayo lakini wakataka kujionea na leo wamekuja wamejionea.
“Kwenye kiwanda hiki cha Knauf uwekezaji unaongezeka mara dufu kwa sababu ya mazingira na mifumo mizuri iliyopo hivyo nitoe rai kwa wawekezaji na wafanya biashara wawekeze kwenye mifumo ya usalama na afya ili kulinda wafanya kazi,” alisema Khadija.
Naye Mwanasheria wa kiwanda cha Knauf, Flora Erasto aliishukuru kamati ya Bunge pamoja na OSHA kwa kufanya ziara kiwandani hapo huku akieleza kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikifanya kazi kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na OSHA tangu kuanzishwa kwake nah ii ndio imetufanya kuwa bora zaidi.
“Kwanza tunaishukuru sana OSHA tangu kuanza kwa kiwanda hiki tumekuwa tukifanya kazi na OSHA vizuri na wamekuwa wakitushauri na kutupa maelekezo muhimu kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi , pia tunaishukuru serikali kwa kutoa miongozo mizuri na nafasi nzuri ambayo imekuwa ikitusaidia sisi kama wawekezaji,” alisema Frola.
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi ni taasisi iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wenye jukumu la kusimamia masuala ya usalama na Afya mahali pa Kazi.