Na Esther Mnyika, Mtazania Digital
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetangaza kuwa utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (Hoima, Uganda – Tanga, Tanzania) umefikia asilimia 47.1 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Julai 2026.
Mradi huu, ambao ni wa kimkakati kwa nchi za Afrika Mashariki, unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania (15%), Serikali ya Uganda (15%), kampuni ya TotalEnergies (62%) kutoka Ufaransa, na kampuni ya CNOOC (8%) kutoka China.
Mratibu wa Mradi kutoka TPDC, Asiadi Mrutu, alisema mradi huo unafuata ugunduzi wa mafuta nchini Uganda, ambako imekisiwa kuwa na mapipa bilioni 6.5 ya mafuta. Mrutu alieleza kuwa sehemu ya mradi unaopita Tanzania ina urefu wa kilomita 1,147 na upana wa mita 30, ambapo wananchi 9,927 wameguswa na mradi huu.
“Kati ya wananchi hao, ni wananchi 344 pekee ambao wamepoteza nyumba zao za makazi, sawa na asilimia 3.4. Kati ya hao, wananchi 50 walichagua kupokea fidia ya fedha taslimu, huku wananchi 294 wakichagua kujengewa nyumba mbadala,” alisema Mrutu.
Malipo ya fidia na ujenzi wa nyumba mbadala
Mrutu alisema kuwa zoezi la utwaaji wa ardhi limezingatia sheria za Tanzania na taratibu za kimataifa ili kuhakikisha haki na usawa kwa wananchi wanaopisha mradi. Kufikia Oktoba 31, 2024, nyumba zote 340 zilizojengwa kwa ajili ya wananchi 294 zimekamilika na kukabidhiwa, na malipo ya fidia kwa wananchi 9,858 yamefanyika, ikiwa ni jumla ya Sh bilioni 35.1 sawa na asilimia 99.3 ya malipo yote yaliyopangwa. Hata hivyo, wananchi 69 wanaendelea kushughulikia changamoto za kumalizia taratibu za kisheria ili kuweza kulipwa fidia zao.
Ajira na ununuzi wa bidhaa za ndani
Tangu mradi huo ulipoanza rasmi Februari 2022, umetoa ajira kwa Watanzania 8,694 kupitia wakandarasi katika maeneo mbalimbali, ambapo inakadiriwa kuwa ajira 7,030 zaidi zitatolewa wakati wa ujenzi wa bomba. Kufikia Septemba 30, 2024, jumla ya Watanzania 6,430 wameajiriwa katika mradi huu. Mrutu alisema kuwa kampuni ya EACOP, ambayo inasimamia mradi huo, inatarajia kuwa na jumla ya wafanyakazi 148 mara baada ya ujenzi kukamilika, ambapo 114 watatoka Tanzania na 34 watatoka Uganda.
Manufaa ya kiuchumi kwa Taifa
Kwa mujibu wa Mrutu, mradi huu umenunua huduma na bidhaa za ndani zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 304.95, sawa na sh bilioni 821.1, hatua inayolenga kuchochea uchumi wa ndani.
“Mradi huu unaendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kupitia ajira, ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani, na kukuza ujuzi wa Watanzania kwenye sekta ya mafuta na gesi,” aliongeza.
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki unalenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji mafuta, huku ukiwa na athari kubwa katika kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii kwa nchi za Tanzania na Uganda.