26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yahimiza wabunifu majengo na wakadiriaji kuchangamkia fursa za miradi mikubwa

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali imetangaza kuendelea kutoa hamasa kwa wataalam wa ubunifu wa majengo na ukadiriaji majenzi ili kuchangamkia fursa za ajira katika miradi mikubwa inayoendelea nchini, hatua inayolenga kukuza sekta ya ujenzi ikiwemo kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Akizungumza katika mkutano wa tano wa Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi uliofanyika Oktoba 29, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, alisema kuwa serikali itaendelea kuthamini na kuwekeza katika taaluma hiyo kwa kutoa tenda za miradi kwa wataalam wa ndani ili kuongeza uzalendo na kuhamasisha maendeleo ya nchi.

“Tumepiga hatua kubwa kutoka tulipotoka, na ni muhimu kwa taaluma hizi kuendelezwa. Tunapaswa kuwashawishi wanafunzi wetu kuanzia shule za msingi, sekondari na vyuoni wapende masomo ya sayansi ili kusaidia nchi yetu kuimarika na kujengeka zaidi,” alisema Mpogolo.

Aidha, Mpogolo aliwataka wataalam wa ndani kuchangamkia fursa za tenda zinazojitokeza badala ya kutegemea wageni kwa kazi hizo, akibainisha kuwa hali hiyo inapaswa kuimarishwa ili kuweza kufikia viwango vya juu vya ubora na kuleta maendeleo endelevu.

Pamoja na hayo, alionya juu ya wataalam wanaojikita zaidi kwenye kutafuta fedha za muda mfupi badala ya kulenga weledi kazini, akisema kuwa mwenendo huu unachangia miradi kutokuwa na ubora unaotakiwa na kupoteza imani ya umma.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch Daud Kondoro, alisema wizara itaendelea kuimarisha sekta ya wabunifu na wakadiriaji majenzi kwa kuwajengea uwezo kupitia mafunzo.

“Wizara ya Ujenzi itatenga fedha kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wataalamu 180 kila mwaka ambao wanahusika na ubunifu wa majengo na ukadiriaji majenzi, ili kujenga uwezo na weledi zaidi katika taaluma yao,” alisema Kondoro.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Dk. Ludigija Bulamile, alieleza kuwa hadi sasa bodi hiyo imesajili wahitimu 873 kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini na inalenga kuhakikisha wahitimu wote wanasajiliwa ndani ya kipindi cha miaka miwili baada ya kuhitimu masomo yao.

Mhandisi Alfayo Khamisi, mmoja wa wahitimu waliotunukiwa vyeti katika mkutano huo, alishukuru kwa kutambuliwa na kuahidi kuwa atafanya kazi zake kwa weledi na kujitolea kwa maendeleo ya taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles