25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 30, 2024

Contact us: [email protected]

Ufaulu Mtihani wa Elimu ya Msingi wapanda kwa asilimia 80.87, NECTA yafafanua

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Ufaulu wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2024 umeongezeka kwa asilimia 80.87, tofauti na mwaka 2023 ambapo ulikuwa asilimia 80.58. Hii inaashiria ongezeko la asilimia 0.29 katika ufaulu wa jumla.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 29, 2024, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Said Mohamed alisema jumla ya watahiniwa 974,229, sawa na asilimia 80.87 ya waliopata matokeo, wamefaulu mtihani huo.

“Ubora wa ufaulu kwa madaraja A na B umeongezeka, ambapo watahiniwa 431,689 sawa na asilimia 35.83 wamepata madaraja hayo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.65 ikilinganishwa na mwaka 2023,” alisema Dk. Mohamed.

Kwa upande wa jinsia, wavulana waliofaulu ni 449,057 sawa na asilimia 81.85, wakati wasichana waliofaulu ni 525,172, sawa na asilimia 80.05. Aidha, kati ya waliopata madaraja ya juu (A na B), wasichana ni 216,568, sawa na asilimia 33.01, huku wavulana wakiwa 215,121, sawa na asilimia 39.21.

Jumla ya watahiniwa na wenye mahitaji maalum

Dk. Mohamed aliongeza kuwa jumla ya watahiniwa 1,230,774 waliosajiliwa kufanya mtihani huo walihusisha wasichana 666,597 sawa na asilimia 54.16 na wavulana 564,177 sawa na asilimia 45.84. Watahiniwa wenye mahitaji maalum walikuwa 4,583, sawa na asilimia 0.37.

Kati ya waliojiandikisha, watahiniwa 1,204,899 sawa na asilimia 97.90 walifanya mtihani, ambapo wasichana walikuwa 656,160 (asilimia 98.43) na wavulana walikuwa 548,739 (asilimia 97.26). Watahiniwa 25,875 sawa na asilimia 2.10 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali.

Ufaulu kwa masomo na ubora wa madaraja

Katika tathmini ya masomo, ufaulu wa somo la Kiswahili ulifikia asilimia 86.58. Kwa upande wa somo la Kiingereza, ufaulu umeimarika na kufikia asilimia 43.48, ikiwa ni ongezeko la asilimia 9.13 ikilinganishwa na mwaka jana.

“Katika somo la Kiswahili, wasichana wamefaulu zaidi kuliko wavulana kwa asilimia 0.36, ilhali kwa somo la Kiingereza wavulana wamefaulu zaidi kwa asilimia 0.25,” alieleza Dk. Mohamed.

Kwa upande wa madaraja A na B, watahiniwa waliopata daraja hizi katika Kiswahili ni asilimia 53.46, huku wale wa Kiingereza wakiwa asilimia 15.25, ikiashiria ongezeko ikilinganishwa na mwaka 2023.

Matokeo yaliyofutwa na matokeo yaliyowekwa kizuizini

Katika hatua nyingine, NECTA ilizuia matokeo ya watahiniwa 418 waliopata changamoto kama ugonjwa au matatizo mengine yaliyowazuia kufanya baadhi au masomo yote. Watahiniwa hao wamepewa nafasi ya kurudia mtihani mwaka 2025 kwa mujibu wa kifungu cha 32(1) cha kanuni za mitihani.

Aidha, Dk. Mohamed alieleza kuwa matokeo ya watahiniwa 45 yalifutwa kwa sababu ya kugundulika kwa udanganyifu katika mtihani, kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(j) cha sheria ya baraza la mitihani, sura ya 107, pamoja na kifungu cha 30(2)(b) cha kanuni za mwaka 2016. Pia, watahiniwa 16 walioandika lugha isiyofaa kwenye skripti zao walipoteza matokeo yao, kwa mujibu wa kifungu cha 17(1) cha kanuni hizo.

Kwa jumla, matokeo haya yanaonesha ongezeko la ufaulu na kuimarika kwa ubora katika baadhi ya masomo, jambo linalochangia katika kuboresha elimu ya msingi nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles