25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yazindua Ofisi kwa walipa kodi binafsi wa hadhi ya juu

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua rasmi Ofisi Maalum kwa Walipa Kodi Binafsi wa Hadhi ya Juu, ikiwa ni hatua ya kuboresha huduma kwa kundi la walipa kodi wenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

Jumla ya walipa kodi 158 wamepata sifa za kuhudumiwa katika ofisi hiyo, wakiwemo wamiliki wa kampuni binafsi 111 ambazo zinaingiza mapato ya Sh Bilioni 20 kwa mwaka.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alitoa maelezo hayo wakati wa uzinduzi wa ofisi hiyo iliyopo katika jengo la Golden Jubilee Tower, akisema kwamba ofisi hiyo inalenga kutoa huduma bora na kuondoa usumbufu kwa walipa kodi wa kundi hili, ambao ni muhimu katika kuchangia pato la taifa.

“Kwa sasa, tunahudumia walipa kodi 158, ambapo wamiliki binafsi wa kampuni ni 111. Wote wamekwisha kualikwa na kupewa maelezo kuhusu huduma hii,” alisema Mwenda. Aliongeza kuwa huduma hii pia inawahusisha viongozi wa mihimili mitatu ya serikali, ambapo tayari viongozi 47 kutoka ngazi za juu wanapata huduma hiyo.

Mwenda alifafanua kuwa huduma hiyo ni kwa ajili ya wale ambao wamiliki wa kampuni zao wanaingiza zaidi ya Sh Bilioni 20 kwa mwaka, wamiliki wa hisa zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2.5, pamoja na washirika katika makampuni yenye faida ya Shilingi Bilioni 20 kwa mwaka.

“Naipongeza sana hatua ya kuwa na wateja 111 wenye sifa za hadhi ya juu katika ulipaji wa kodi. Viongozi hawa 47 nao wamepata hadhi hii kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa, na tutahakikisha wanapata huduma stahiki na zinazoendana na nafasi zao,” aliongeza Mwenda.

Kamishna Mkuu alieleza kuwa makundi haya yamepewa kipaumbele kutokana na mchango wao mkubwa katika ajira na maendeleo ya kampuni zao. Pia, viongozi wa ngazi za juu wamepewa fursa hiyo kwa kuwa na majukumu mengi yanayohitaji uangalizi maalum.

Mwenda alisisitiza kwamba, lengo sio kuwatoza kodi kubwa, bali kuhakikisha wanalipa kodi inayostahili na kwa wakati. “Tutaendelea kutoa elimu na kuwapa usaidizi walipa kodi hawa ili kuwa na ufahamu zaidi kuhusu majukumu yao ya kikodi,” alisema.

TRA ina matumaini kwamba kupitia ofisi hii mpya, itakuwa rahisi kwa walipa kodi wa hadhi ya juu kutekeleza majukumu yao bila usumbufu, na hivyo kuendelea kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles