25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mchengerwa awataka wakuu wa mikoa kusimamia sheria na kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amewaagiza wakuu wa mikoa kote nchini kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kusimamia sheria, kanuni, na taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Baadhi ya Watumishi wa halmashauri ya jiji la Mwanza, wananchi na waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri Mohammed Mchengerwa (hayupo pichani)

Waziri Mchengerwa pia ameonya kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya vyama vya siasa ambavyo vitasababisha taharuki au kuharibu uchaguzi huo.Akizungumza leo jijini Mwanza mbele ya watumishi wa halmashauri ya jiji, wananchi, na waandishi wa habari, Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa vyama vya siasa kuweka mbele maslahi ya wananchi na kuhakikisha kuwa wanafanya shughuli zao kwa kuzingatia amani na sheria ili wananchi waweze kutekeleza haki yao ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa bila vikwazo.

“Ninawaelekeza wakuu wa mikoa kote nchini kuhakikisha kwamba wanasimamia kanuni, taratibu, na miongozo ya uchaguzi huu,” alisema Waziri Mchengerwa. Aliongeza kwa kutoa rai kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea na ufuatiliaji wa kina ili kukabiliana na changamoto zozote za kiusalama zitakazojitokeza.

Aidha, amewataka wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa. Waziri Mchengerwa alikanusha taarifa zinazodai uwepo wa vituo bubu vya uandikishaji vilivyolenga kuhujumu uchaguzi huu, na akasisitiza kuwa zoezi la uandikishaji linaendelea kwa uwazi na kwa kufuata sheria.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wakurugenzi Tanzania bara, Wakili Msomi Kiomoni Kibamba, ambaye pia ni Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Mwanza, ameahidi kuwa wakurugenzi hawatosita kuchukua hatua kali dhidi ya wale watakaobainika kuharibu zoezi la uandikishaji na uchaguzi.

Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, hadi kufikia Oktoba 14, zoezi la uandikishaji ambalo lilianza Oktoba 11 lilikuwa limefikia asilimia 45 ya walengwa nchi nzima, huku mkoa wa Tanga ukiongoza kwa kiwango cha uandikishaji. Zoelo hili linatarajiwa kumalizika Oktoba 20, na Waziri Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa vyama vya siasa na wadau wote kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles