26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mnada wa kwanza wa korosho Tandahimba na Newala wafana

*Wakulima wamshukuru Rais Samia

Na Mwandisgi Wety, Mtanzania Digital

Leo, Oktoba 11, 2024, historia mpya imeandikwa katika mikoa ya kusini baada ya kufanyika mnada wa kwanza wa korosho ulioandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU).

Mnada huo, uliofanyika katika Halmashauri ya Mji wa Newala, umeshuhudia jumla ya tani 3,857 za korosho zikiuzwa kwa bei ya juu ya shilingi 4,120 kwa kilo na bei ya chini ya shilingi 4,035. Mafanikio haya yameleta matumaini mapya kwa wakulima wa korosho ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakihitaji bei nzuri kwa zao hili muhimu.

Wakulima wa Tandahimba na Newala wamefurahia hatua hii, huku wakimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuhakikisha kuwa bei za korosho zinaimarika na kuwa na tija kwa wakulima.

“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa juhudi zake za kuhakikisha tunapata bei nzuri kwa mazao yetu. Hii ni hatua kubwa kwa wakulima wa korosho, na tunaamini kwamba serikali itaendelea kutusaidia ili tuendelee kuuza kwa bei nzuri kama hii,” alisema mmoja wa wakulima mara baada ya mnada.

Wakulima hao wameiomba serikali kuendelea kusimamia bei hizi katika minada ijayo, wakiamini kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia, sekta ya kilimo cha korosho itaendelea kuimarika na kuwapatia manufaa makubwa. Mnada huu umeleta nuru mpya kwa wakulima wa mikoa ya kusini ambao hutegemea korosho kama chanzo kikuu cha mapato.

Meneja wa TANECU, Mohamedi Nassoro Mwinguku, aliipongeza serikali kwa kushirikiana nao na kuahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na wakulima ili kuhakikisha wanapata faida zaidi kupitia mazao yao.

“Huu ni mwanzo mzuri kwa msimu huu wa korosho, tunatarajia kuona mafanikio zaidi katika minada ijayo. Tunaendelea kuwahimiza wakulima wetu kuongeza uzalishaji na kuzingatia ubora wa mazao yao,” alisema Mwinguku.

Hatua hii ya kupandisha bei ya korosho inadhihirisha dhamira thabiti ya serikali ya kuimarisha sekta ya kilimo na kuhakikisha wakulima wanapata bei bora za mazao yao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia ameendelea kusisitiza kwamba serikali yake itaboresha maisha ya wakulima kwa kuweka mazingira rafiki ya soko la mazao, hasa katika mikoa ya kusini kama Mtwara na Lindi.

Wakulima sasa wanatarajia kuwa na msimu wenye mafanikio zaidi na kuimarisha hali zao za kiuchumi kupitia zao hili la korosho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles