27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Lukuvi atoa hakikisho la uchaguzi huru na wa haki wa serikali za mitaa na ule wa 2025

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, amewatoa hofu wananchi kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ujao, akisisitiza kuwa uchaguzi huo utafuata sheria na kanuni zote na kwamba kila raia anastahili kushiriki kikamilifu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 7, 2024, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu, Waziri Lukuvi alieleza lengo la ziara hiyo kuwa ni kujitambulisha kwa ofisi za vyama hivyo na pia kuwa na mazungumzo yenye kujenga.

“Nawaondoa hofu wananchi kuhusu uchaguzi ujao,” alisema Lukuvi. “Kinachotakiwa ni kushiriki katika kupiga kura, na wakati wa kampeni hakikisheni mnasikiliza kwa makini sera na hoja za kila chama husika.”

Aliwataka viongozi wa vyama hivyo kuwahamasisha wanachama wao kushiriki katika uandikishaji wa daftari la wapiga kura na kuhakikisha wanapiga kura siku ya uchaguzi. Aidha, aliwahimiza viongozi wa vyama hivyo kuzingatia maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyetoa miongozo ya 4R ambayo ni: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi, na Kujenga upya taifa.

Siasa za amani na kujenga Taifa

Lukuvi pia alisisitiza umuhimu wa siasa zinazojenga na zenye tija kwa manufaa ya wananchi, akibainisha kwamba, “Vitisho vya watu binafsi siyo vya Serikali, bali ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunaendesha siasa kwa amani. Ingempendeza sana iwapo vyama vitashindana kwa sera na hoja ili wananchi wapate nafasi nzuri ya kuwachambua wagombea na kufanya uamuzi bora.”

Aidha, Lukuvi alibainisha kuwa Rais Dk. Samia ana dhamira ya kuona chaguzi zote nchini zinakuwa huru na haki, akisema, “Chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, uchaguzi ujao utazingatia kanuni na sheria, na hautakuwa na upendeleo.”

Jaji Francis Mutungi apigia chapuo ziara ya Lukuvi

Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa, alisifu juhudi za Waziri Lukuvi, akisema kwamba utaratibu aliouanzisha unaleta umoja na kuviweka vyama pamoja kwa lengo la kuimarisha siasa zenye maadili. “Utaratibu ulioanzishwa na Waziri Lukuvi unaonesha utawajenga wanasiasa kuwa wamoja kwa lengo la kujenga nchi yetu,” alisema Mutungi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Pili Bara wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, alimshukuru Waziri Lukuvi kwa kutembelea ofisi zao, akisema, “Ziara yake hii inajenga umoja na ushirikiano ndani ya vyama vya siasa.”

Viongozi wa Vyama wafurahishwa na ziara

Mwenyekiti wa CHAUMA, Hashim Rungwe, alieleza kufurahishwa kwake na ziara ya Waziri Lukuvi, akisema, “Ni mara yangu ya kwanza kuona waziri anatembelea ofisi za vyama tofauti; jambo hili linatia moyo na linaonesha mshikamano.”

Ziara hiyo iliendelea kwa kutembelea vyama vya ACT-Wazalendo, CHAUMA, UPDP, na CCK. Ziara hiyo itaendelea leo kwa kutembelea vyama vya UDP, NCCR–Mageuzi, CUF, na NLD.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles