26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia aunda Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi

-Lengo ni kuboresha Mfumo wa Kikodi

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa kiongozi wa kwanza tangu enzi za Rais Benjamin Mkapa kuboresha kwa kiasi kikubwa mfumo wa kodi nchini Tanzania, baada ya kuunda rasmi Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi. Tume hii inalenga kuboresha ukusanyaji wa kodi na kuhakikisha ufanisi katika matumizi yake, pamoja na kushughulikia changamoto zinazoathiri mfumo wa kodi nchini.

Akizungumza leo Oktoba 4, 2024, katika hafla ya uzinduzi wa tume hiyo Ikulu, Jijini Dar es Salaam, Rais Dk. Samia alielezea umuhimu wa marekebisho hayo kwa ukuaji wa uchumi wa nchi. Alisema kuwa ni watu milioni mbili tu kati ya Watanzania milioni 65 ndio wanalipa kodi, idadi ambayo ni ndogo mno ikilinganishwa na mahitaji ya maendeleo ya nchi.

“Ni muhimu kwa Watanzania wengi zaidi kushiriki katika kulipa kodi ili kuchangia uchumi wa Taifa,” alisema Rais Samia, akisisitiza kuwa mfumo wa kodi unapaswa kuwa jumuishi zaidi na wenye uwazi kwa faida ya wote.

Rais Dk. Samia alieleza kuwa lengo la tume hiyo ni kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa kodi, jambo ambalo litajenga imani zaidi kati ya wananchi na serikali. “Uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma ni suala muhimu sana, hususan wakati ambapo mfumo wa kodi umekuwa ukikabiliwa na malalamiko kuhusu ubadhirifu na matumizi mabaya ya rasilimali za umma,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Rais Samia, tume hiyo itazingatia mbinu mpya za ukusanyaji wa kodi ili kuongeza mapato ya serikali bila kuongeza mzigo kwa wananchi. Mojawapo ya njia zinazotarajiwa ni matumizi ya teknolojia za kisasa, kama vile mifumo ya kielektroniki, ambayo itarahisisha malipo ya kodi na kuondoa urasimu.

Aidha, Rais Samia aliweka bayana kuwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi utakuwa muhimu katika kufanikisha maboresho haya ya kodi. “Tutashirikiana na sekta binafsi ili kuleta mawazo mapya na mbinu za kisasa za ukusanyaji kodi, huku tukihakikisha mazingira ya biashara yanaboreka na kuvutia zaidi wawekezaji,” alisisitiza.

Rais Samia alihitimisha kwa kueleza kuwa maboresho haya yatasaidia kuongeza mapato ya ndani ya nchi na kuweka msingi thabiti wa kufikia malengo ya maendeleo, hasa katika kipindi hiki ambacho uchumi wa dunia unakabiliwa na changamoto mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles