25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Watahiniwa 1,280,780 kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kesho

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Jumla ya watahiniwa 1,280,780 wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, kati yao wavulana ni 564,176 sawa na asilimia 45.84 na wasichana ni 666,604 sawa na asilimia 54.16.

Kati ya watahiniwa1,280,780 waliosajiliwa kufanya mtihani mwaka huu, watahiniwa1,158,862 sawa na asilimia 94.16 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 71,918 sawa na asilimia 5.84 watafanya kwa lugha ya kingereza waliyokuwa wakiitumia katika kujifunza.

Akizungumza leo Septemba 10, 2024 jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Said Mohamed alisema jumla ya shule 18,964 zitafanya mtihani huo nchini kuanzia kesho na keshokutwa jumla ya masomo sita yatatahiniwa ambayo ni Kiswahili, Kingereza, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, Uraia na Maadili.

Pia alisema watahiniwa wenye mahitaji maalumu waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 4,583 kati yao 98 ni wasioona, 1,402 wenye uoni hafifu, 1,067 wenye uziwi, 486 wenye ulemavu wa akili na 1,530 wenye ulemavu wa viungo.

“Mtihani huu ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa kuwa hupima maarifa na umahiri wa wanafunzi kwa masomo waliyosoma katika elimu ya msingi na matokeo ya mtihani huu hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari hivyo ni muhimu kwa wanafunzi, wazazi na jamii nzima nchini,”alisema.

“Maandalizi yote ya mtihani huo yamekamilika ikiwa kusambazwa kwa karatasi za mitihani na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani katika halmashauri na manispaa zote nchini. Maandalizi kwa watahiniwa wenye mahitaji maalumu yamefanyika ipasavyo,” alisema.

Alisema kamati za mitihani mikoa na halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu kwa kutoa semina kwa wasimamizi wa mtihani na kuhakikisha mazingira ya vituo vya mtihani yanakuwa salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu kutokea.

Dk. Mohamed alizitaka kamati hizo zihakikishe usalama wa vituo vyote vya mtihani unaimarishwa na vituo hivyo vinatumika kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na NECTA.

Aliwataka wasimamizi wa mtihani kufanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini , uadilifu wa hali ya juu, weledi na kwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa ili kila mtahiniwea apate haki yake.

“Baraza linaamini walimu wamewaandaa vizuri watahiniwa wote kwa kipindi cha miaka saba, hivyo matarajio ya Baraza la Mtihani kuwa watahiniwa watafanya mtihani kwa kuzingatia kanuni za mtihani.

“Baraza halihitaji kuona mwanafunzi yeyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu, atakayebainika kufanya udanganyigu matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mtihani,” alisema.

Aidha aliwataka wamiliki wa shule kutambua shule zao ni vituo maalumu vya mitihani, hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mtihani huo.

Vilevile wakuu wa shule watekeleze majukumu yao ya usimamizi kwa kuzingatia mwongozo wa usimamizi uliotolewa na NECTA kuepuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba vya mtihani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles