26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

OSHA yawakumbusha waajiri, wafanyakazi umuhimu wa usalama na afya kazini

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umeelezea umuhimu wa kulinda uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika rasilimali watu kuanzia wanapozaliwa hadi kufikia hatua ya kuajiriwa au kujiajiri katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiwasilisha mada kwenye semina ya waajiri na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) inayofanyika Jijini Arusha Agosti 26 hadi 29, 2024.

Umuhimu huo umeelezwa na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu masuala ya Usalama na Afya kazini katika semina ya waajiri na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) inayofanyika Jijini Arusha kuanzia Agosti 26 hadi 29, 2024.

Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA amesema hadi kufikia hatua ya mtu kuwa na ujuzi fulani na kuajiriwa ama kujiajiri, serikali inakuwa imewekeza kwa kiwango kikubwa ikiwemo kugharamia huduma za afya tangu utotoni pamoja na kumpatia elimu ya kumwezesha kupambana na mazingira yake.

“Serikali yetu inawekeza fedha nyingi katika kuwahudumia watu wake tangu akina mama wanapokuwa wajawazito, wanapojifungua na kulea watoto wao ikiwemo kuwapatia elimu katika ngazi tofauti,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA na kuongeza:

“Kwa mantiki hiyo serikali inategemea kupata faida ya uwekezaji uliofanyika kwa watu wake (return on investment) kupitia watu hao kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kipindi kirefu. Jambo ambalo litawezekana tu endapo wafanyakazi katika sehemu za kazi watalindwa dhidi ya vihatarishi vya magonjwa, ajali na vifo vinavyoweza kutokea katika sehemu za kazi.”

Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Joel Kaminyoge, akifunguasemina ya waajiri na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) inayofanyika Jijini Arusha kuanzia Agosti 26 hadi 29, 2024.

Hivyo, Mtendaji Mkuu wa OSHA ametoa wito kwa waajiri na wafanyakazi kuhakikisha kwamba katika sehemu zao za kazi kunakuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya ikiwa ni pamoja na kuzingatia taratibu zote muhimu za usalama na afya kama inavyoelekezwa na wataalam kutoka katika Ofisi yake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE, Joel Kaminyoge, ameeleza jinsi wanavyoshirikiana na OSHA katika kutoa elimu ya masuala ya usalama na afya kwa waajiri na wafanyakazi nchini hususan wanachama wa TUGHE.

“OSHA ni wadau wetu wakubwa sana ambao mbali na kufadhili shughuli zetu mbalimbali wamekuwa wakishirikiana nasi katika kutoa elimu ya usalama na afya kwa wanachama wetu katika mikutano yetu kama huu unaoendelea hapa Jijini Arusha,” ameeleza Comred Kaminyoge.

Akielezea umuhimu wa semina mbalimbali wanazofanya kwa waajiri na viongozi wa matawi ya TUGHE, Kaminyoge, amesema semina hizo zimesaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi pamoja na kupunguza migogoro mahali pa kazi.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) iliyokabidhiwa wajibu wa kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake. Kupitia sheria hiyo maeneo yote ya kazi nchini yanapaswa kusajiliwa na OSHA na kuingizwa katika utaratibu wa ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya unaofanywa na OSHA kila mwaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles