Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamisi amesema Serikali itaendeleza kampeni za hamasa kwa jamii ili kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030.
Khamis ametoa rai hiyo Agosti 11, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa bonanza la michezo lilioandaliwa na Balozi wa Mazingira Grit Mwimanzi kwa kushirikiana na Umoja wa Vilabu vya Mazoezi Kata ya Vingunguti (UVIJOVI), ambalo lililenga kuhamasisha jamii umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na uhifadhi wa mazingira.
Amesema umuhimu wa agenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inasukumwa zaidi na ongezeko la athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia ikihusisha kuni na mkaa.
“Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni agenda mahususi ambayo imechukua nafasi kubwa katika Serikali ya Awamu ya Sita…Kama mnavyoshuhudia Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara kwa kuhakikisha agenda hii inapata msukumo mkubwa katika jumuiya ya kimataifa,” amesema Naibu Waziri Khamis.
Ameeleza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais tayari imeandaa mikakati mbalimbali ya uhamasishaji ikiwemo mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia uliofanyika mwaka 2022 ambao tayari umetoa mwelekeo wa kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.
Amesema nishati safi ya kupikia inatambulika kuwa salama, nafuu, endelevu na inayopatikana kwa urahisi na hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuhimiza jamii kuachana na nishati chafu ambayo ina kiwango kikubwa cha sumu sambamba na uzalishaji gesi joto.
Kwa mujibu wa Khamis ameeleza utaratibu wa upatikanaji wa nishati isiyo safi ya kupikia inahusishwa moja kwa moja na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa, hivyo kuchangia kuongezeka kwa ukame na athari za mifumo ya kiikolojia.
Akifafanua kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi na taasisi za utafiti ili kuongeza wigo wa teknolojia za kutosha katika nishati, vifaa na mifumo ya kibiashara ili kupunguza gharama za nishati safi ya kupikia.
Aidha ameongeza kuwa Tanzania itaendelea kuongoza jitihada za kitaifa, kimataifa na kikanda za kuhakikisha kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia inakuwa agenda ya kudumu na kuwahimiza wananchi kuunga mkono juhudi hizo za Serikali.
Katika hatua, nyingine, amewataka wananchi kuacha kuvamia na kuharibu vyanzo vya maji kwa kuendesha shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo ambapo husababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na mifumo ya ikolojia.
“Tuendelea kuelimisha wananchi juu ya upandaji miti rafiki wa mazingira na kuepuka kilimo kandokando ya mito ili kulinda mazingira yetu. Wananchi ndio walinzi na wahifadhi wa kwanza katika kutunza Mazingira” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewahimiza wananchi wa wilaya hiyo umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira na kutoa hamasa kwa jamii kujenga utamaduni wa upandaji miti na kushiriki zoezi la usafi wa mazingira linalofanyika kila jumamosi ya mwisho wa mwezi.
“Suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira na kila mmoja wetu, nawasihi tuendelee kujitokeza na kushiriki katika upandaji miti na pia tuhamasishe jamii kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ili kuunga mkono juhudi za serikali” amesema Mpogolo.
Naye Balozi wa Mazingira, Mwimanzi ameutaka UVIJOVI kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii na wananchi wa Kata ya Vingunguti umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kulinda mazingira na afya za Watanzania.