Na Mwandishi Wetu, Katavi
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (Mb), Julai 20, mwaka huu ameendelea na ziara yake ya kikazi kwa kukagua mradi wa ukarabati wa skimu ya umwagiliaji ya Usense, mkoani Katavi, na kuzungumza na wanakijiji wanufaika wa mradi huo.
Mradi wa Usense unahusisha eneo la hekta 106 ambapo Waziri Bashe alieleza malengo ya Serikali ya kuboresha na kuongeza huduma kwa ustawi wa jamii. Malengo haya yanajumuisha ujenzi wa awamu mbili wa mfereji na bwawa la maji kwa ajili ya umwagiliaji wa kilimo.
Katika hatua ya kufanikisha awamu hizo, Waziri Bashe alimuelekeza, Raymond Mndolwa, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), kujenga daraja la kivuko ili kurahisisha shughuli za kilimo kwa wakulima, ambao kwa sasa wanalazimika kutembea kilomita 7 badala ya 1.8.
Waziri Bashe pia aliwasihi wanakijiji kutouza ardhi yao ili miradi hiyo iwe na manufaa kwa familia zao na vizazi vijavyo. Aidha, Waziri Bashe ataendelea na ziara yake mkoani Kigoma Julai 21, 2024, ambapo atakagua mradi wa umwagiliaji wa Lueche.