Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Serikali imelipongeza Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwa kujiimarisha kwenye misingi ya makuzi ya vijana na watoto na kulifanya kuwa endelevu.
Kanisa hilo limehitimisha sherehe za maadhimisho ya miaka 85 tangu lilipoanzishwa mwaka 1939 na Wamisionari kutoka Marekani.
Akizungumza leo Julai 14,2024 wakati wa kilele cha maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesema mkakati wa TAG wa kuwajenga watoto kiimani na kimakuzi kwa kufuata taratibu za kidini ndio maandalizi mazuri ya kuwa tegemeo la nchi kwa baadaye.
“Kanisa hili ni mfano katika kukuza umoja na ushirikiano kati ya wakristo na waumini wengine, Rais Samia anatambua na kuthamini ushirikiano uliopo baina ya kanisa na serikali, tuna kila sababu ya kuwashukuru kwa kazi kubwa mnayoifanya…TAG mmeendelea kukemea maovu na mmomonyoko wa maadili,” amesema Majaliwa.
Majaliwa pia amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kuboresha tarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kujiweka tayari kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye nchini.
Waziri Mkuu pia amempongeza Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali, kwa utendaji mzuri na ubunifu alionao katika kuliongoza kanisa hilo na kuahidi kuendelea kumpa ushirikiano wakati wote.
Naye Askofu Dk. Mtokambali amesema wanamshukuru Mungu kwa kuliongoza vema kanisa hilo, kuliwezesha kutimiza maono na mikakati mbalimbali waliyonayo na kulilinda katika kipindi chote tangu lilipoanzishwa.
“Kanisa limepambana na maadui wa ndani na nje na wameshindwa, kanisa limebaki imara. Ili Mungu aendelee kutembea nasi lazima tuendelee kuwa na maono na kufanya makubwa. Tuendelee kuwa na umoja, upendano na mshikamano, tuwakatae wote wanaotugawa ili kanisa la TAG libaki kuwa na umoja na mshikamano…tuendelee kujitoa na kujituma kwa hali na mali,” amesema Askofu Dk. Mtokambali.
Amesema mkakati wa kanisa hilo ni kuwapa kipaumbele watoto na vijana kwa sababu ndio rasilimali watu itakayowezesha kufika miaka mingine 85.
Kwa mujibu wa Dk. Mtokambali, uwepo wa idara ya vijana na watoto tangu kuanzishwa kwake kumesaidia kuratibu, kuhamasisha na kulea kundi hilo na hata viongozi wengi wanaofanya vizuri katika ngazi mbalimbali ni zao la idara hizo.
Dk. Mtokambali pia ameipongeza Serikali kwa kazi inayofanya ya kuiletea nchi maendeleo hasa katika sekta ya mundombinu.
“Nimekuwa nikisafiri kwa mabasi kuja ofisini Dar es Salaam, imekuwa inanichosha kukaa masaa manne mpaka matano barabarani, lakini nilipokuja kwenye maadhimisho haya nilitoka Morogoro saa 1:30 usiku hadi saa 3:30 usiku nilikuwa Dar es Salaam. SGR imeniletea raha, sasa nitapunguza masaa matatu ya safari kwenda Dodoma na kuja Dar es Salaam…haya ni maendeleo,” amesema Askofu Dk. Mtokambali.
Askofu Mkuu huyo wa TAG pia ameipongeza Serikali kwa kudumisha amani na umoja pamoja na uhuru wa kuabudu uliowezesha kanisa hilo na madhehebu mengine kupiga hatua kubwa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TAG, Mchungaji Joseph Marwa, amesema kwa miaka minne tangu waanze kutekeleza mpango mkakati wa pili (2020 – 2033) kumekuwa na ongezeko la makanisa na watumishi.
Amesema makanisa mapya 5,918 yameanzishwa, wachungaji wapya 5,804, wainjilisti wapya 360, majimbo mawili mapya na wilaya za kikanisa zimeongezeka kutoka 557 hadi 860.
Katika sekta ya elimu amesema wana shule za chekechea 117, msingi 17, sekondari 7 huku nane zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi, vyuo viwili vya ualimu, vituo 89 vya watoto yatima vinavyohudumia watoto 14,000 na vyuo vitano vya ufundi kimoja kikiwa kinajengwa mkoani Manyara.
Kwa upande wa vituo vya afya amesema kwa sasa vimefikia vinane ambapo kila kimoja kinahudumia wastani wa wagonjwa 200 kwa siku na visima vya maji vimeongezeka kutoka 153 hadi kufikia 293.
Katibu Mkuu huyo amesema katika maadhimisho ya miaka 85 visima 17 vya maji vimechimbwa katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambavyo vinahudumia watoto zaidi ya 15,400.