25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Kikwete aipongeza WHI kwa kupunguza changamoto ya Nyumba kwa Watumishi wa Umma

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete, ametembelea banda la Watumishi Housing Investment (WHI) katika Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) na kuwasifu kwa juhudi zao katika kupunguza changamoto ya nyumba kwa watumishi wa umma.

Akiwa katika banda hilo juzi, Dk. Kikwete alieleza kuridhishwa kwake na hatua kubwa zilizofikiwa na Watumishi Housing Investment katika kuboresha makazi ya watumishi wa umma. Alisema kuwa juhudi hizo zimeleta mabadiliko makubwa na kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la upatikanaji wa nyumba bora kwa watumishi hao.

“Nimefurahishwa sana na kazi nzuri inayofanywa na Watumishi Housing Investment. Kwa sasa, changamoto ya nyumba kwa watumishi wa umma imepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma wakati taasisi hii inaanza. Hili ni jambo la kupongezwa sana,” alisema Dk. Kikwete.

Upande wake, Afisa Masoko wa WHI, David Mwaipaja, kando na kumshukuru Dk. Kikwete kwa kutembelea banda lao, pia alimweleza kuwa wamejenga nyumba nyingi kwa ajili ya watumishi wa umma katika maeneo mbalimbali nchini, huku wakihakikisha zinapatikana kwa bei nafuu na kwa masharti rahisi ya malipo.

“Tunaendelea na juhudi zetu za kuhakikisha kila mtumishi wa umma anapata nyumba bora na kwa bei nafuu. Kwasasa tuna nyumba katika Mradi wetu wa Kisasa Relini ambapo tumejenga nyumba za kisasa za ghorofa zenye jumla ya nyumba 60 zilizogawanywa katika majengo manne zilizopo katika eneo la Njendengwa mjini Dodoma. Nyumba hizi zinajengwa na kusimamiwa na Watumishi Housing Investments (WHI) hivyo tunawakaribisha sana watumishi kuchangamkia nyumba hizi,” alisema Mwaipaja.

Ziara ya Dk. Kikwete katika banda la Watumishi Housing Investments imeleta hamasa kubwa na kuonyesha umuhimu wa juhudi zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuboresha maisha ya watumishi wa umma nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles