NI simulizi zinazohusu ubabe wa Pablo Emilio Escobar, aliyetoka familia ya mwalimu na mkulima, alivyoanza uhalifu, alivyojitengenezea utajiri, maisha yake mafupi ya kisiasa, asivyoruhusu chochote kikatize kwenye himaya yake na namna mamlaka za Colombia zikishirikiana na Marekani zilivyogundua njia pekee za kumkabili ni kutumia wahalifu pamoja na ‘kuishikilia mateka’ familia yake.
Licha ya kuwa alikuwa mhalifu, machoni pa umma hasa watu wa kada la chini alikuwa mhisani na shujaa mkubwa, si tu nchini mwake Colombia bali pia nje ya mipaka ya taifa hilo ikiwamo Marekani iliyokuwa ikimwinda kwa muda mrefu.
Anaaminika kuwa ndiye mhalifu tajiri zaidi na wakati huo huo mhisani mkubwa, ambaye hakuwahi kutokea katika historia ya dunia, akiwa amejenga maelfu ya makazi katika vitongoji masikini, miundo mbinu isiyo na idadi kuanzia shule, hospitali, makanisa, viwanja vya michezo, barabara na kila aina ya misaada.
Katika toleo la wiki kwa wiki ya pili mfululizo tuliendelea na yaliyojiri katika siku isiyosahaulika Colombia ya Alhamisi ya Desemba 2, 1993, ambapo Escobar yu mafichoni akimsaidia mwanae kujibu maswali aliyopewa na mwanahabari, lakini pia kikosi cha polisi cha kunasa mawasiliano Colombia kinahisi kubaini hapo alipo. Sasa endelea………
Wakati Luteni Hugo akijaribu kubaini unakotoka mlio wa simu wa Escobar, kinara huyo wa unga duniani alikuwa akiendelea na mazungumzo na mwanawe Juan.
Juan Pablo alirudia swali kutoka orodha ya maswali 40 aliyopewa na mwandishi wa Colombia.
Yeye na baba yake waliendelea kutengeneza majibu ya maswali hayo.
Swali la sasa liliuliza kwanini mataifa mengineyo pia yalikataa kuruhusu Juan Pablo, mama na dada yake kuingia katika ardhi zao.
Familia hii iliishi chini ya vitisho vya kuuawa na genge la visasi la wanamgambo wa Los Pepes, hivyo ilitamani sana kuikimbia Colombia.
“Nchi hizo zilitukatalia kuingia kwa sababu hazifahamu ukweli,” Escobar alisema, akimjibua mwanawe swali hilo.
“Ndiyo,” Juan Pablo alikubaliana nalo huku akiandika notisi wakati baba yake akizungumza.
“Tunatarajia kubisha hodi kwa kila ofisi za ubalozi duniani kwa sababu tumedhamiria kupambana katika hili,” Escobar aliendelea.
“Kwa sababu tunataka kuishi na kusoma katika nchi nyingine bila walinzi na pengine tukiwa na majina mapya.”
“Sawa kabisa, kama ujuavyo baba,” Juan Pablo alitaka kumtaarifu baba yake kitu kipya.
“Nilipokea simu kutoka kwa mwandishi huyu akinitaarifu Rais Alfredo Cristiano kutoka Ecuador, hapana, nadhani ni kutoka El Salvador . . .”
“Unasema kweli?” Escobar aliuliza huku akiondoka na kuhamia katika dirisha la gorofa ya pili, baada ya kubaini mazungumzo hayo yalichukua dakika kadhaa.
Alikuwa amejiwekea ukomo wa kuzungumza kwa muda mfupi ili kutonaswa.
Wakati akisikiliza ‘taarifa njema’ za mwanawe, akapepesa macho kuelekea nje kuangalia magari yaliyokuwa yakipita mtaani.
“Ndiyo, amejitolea kutupokea. Nilisikia kauli vyema na aliniunganisha na simu,”Juan alimhakikishia baba yake.
“Dah.Kweli?, Pablo aliuliza kana kwamba haamini habari hizo ‘nzuri.’
“Na alisema kuwa kwa namna fulani iwapo hilo litachangia amani kwa nchi, atakuwa tayari kutupokea, kwa sababu dunia hupokea madikteta na watu wabaya, kwanini isiwe sisi?”
“Sawa, tusubiri na kuona kwa sababu nchi hii imefichwa kidogo.”
“Naam, lakini kuna uwezekano na ni taarifa kutoka kwa rais.”
“Tazama, kwa heshima ya El Salvador,” Escobar alisema.
“Yeah?”
“Iwapo wataulizia kitu chochote, waambie familia inashukuru sana na inaheshimu maneno ya rais, kwamba anafahamika kuwa rais wa amani nchini El Salvador.”
“Yeah.”
Escobar alikaa dirishani, akiwa na wasiwasi kutokana na urefu wa mazungumzo ya simu aliotumia siku hiyo.
Hakika haukuwa wasiwasi wa bure!
Wakati Juan Pablo alipouliza swali kuhusu familia kuwa chini ya ulinzi wa serikali, baba yake alijibu haraka haraka:
“Wewe unaweza kulijibu hilo.”
Juan Pablo aliwasilisha maswali matatu zaidi, lakini baba yake alisitisha ghafla mazungumzo. Alikuwa ameona kitu fulani mtaani.
“OK, tusubiri hilo kwa siku nyingine,” Escobar alisema.
“Yeah, OK,” Juan Pablo alisema. “Siku njema.”
“Nawe pia.”
“Yeah.”
Mawimbi ya redio yalimuelekeza Luteni Hugo Martinez asonge mbele moja kwa moja.
Mstari katika skrini ya kompyuta yake ulirefuka na sauti katika vipokea sauti (headphones) vyake ilizidi kuwa na nguvu zaidi wakati gari lake la polisi lisilo na alama lilipopita mtaani katika kitongoji cha tabaka la kati cha Medellin siku ile ya Desemba 2, 1993.
Hugo na dereva wake walijaribu kutafuta nyumba, ambayo sauti hiyo ilikuwa ikitokea.
Waliendesha kuelekea chini ya mtaa hadi ishara ilipofikia katika kilele na kuanza kupungua ukubwa.
Mstari ulipotea katika pembe ya skrini na sauti kupungua.
Waligeuza gari na kurudi walikotoka na kwa kufanya hivyo, mstari ulichomoza tena taratibu na kwa mara nyingine ukatanda kwa uwazi katika skrini.
Wakasimama. “Ni hapa,” Hugo alisema. Kisha baada ya muda wakaendelea mbele kupita mahali hapo ili kuhakikisha iwapo wako sahihi.
Kwa mara nyingine ishara ilifikia katika kilele chake na taratibu ikaanza kupungua ukubwa wake.
Dereva aligeuza gari tena kurudi walikotoka. Walipoifikia nyumba ambayo kila wanapoikabili ishara huwa na nguvu zaidi, Hugo alitazama mbele kuelekea nyumba hiyo na kumuona mwanamume mnene aliyekuwa amesimama katika dirisha la gorofa ya pili.
Alikuwa na nywele ndefu nyeusi zenye mawimbi na ndevu nyingi. Picha hiyo ilipenya ndani ya mwili wa Hugo mithili ya shoti ya umeme.
Bila kujali wingi wa nywele na ndevu, ambazo zinaweza kuwa bandia, kwa utaalamu wao polisi waliandaa michoro tofauti tofauti kuonesha Escobar anakua kuaje anapojibadili uso.’
Hakika ilikuwa taswira ya Pablo Escobar, ilikuwa kidogo Hugo apayuke.
Pablo alikuwa akizungumza kwenye simu. Mara akamuona akirudi kinyumenyume kutoka dirishani.
Hugo akabaini kwamba kinara huyo wa unga duniani alishtuka kwa mshangao.
Kupitia head phones, alimsikia Escobar akisema ‘Siku njema,” na kuhitimisha mazungumzo na mwanawe.
Hilo lilizidi kumhakikishia Hugo kuwa huyo ni Pablo wa ukweli na kitendo cha kurudi nyuma kutoka dirishani na kisha kusikika akikata simu, kinadhihirisha alibaini tayari anafuatiliwa.
Hugo na timu yake walikuwa wamemfuatilia hapo Escobar kwa siku tatu wakati akizungumza kwa simu na mkewe na mwanawe hotelini mjini Bogota.
Kinara huyo wa unga alikuwa akijaribu kuiondoa salama familia yake kutoka Colombia.
Hadi wakati huo maofisa hawakuwa wakijua wapi mawasiliano yake ya simu yalikuwa yakitokea.
Miaka mingi ya juhudi za kumtafuta, maelfu ya uhai ukipotea, uvamizi wa maelfu wa polisi uliokosa mafanikio, mamilioni ya dola yaliyopotea kumsaka.
Mabilioni, ambayo kiasi chake hakifahamiki na kamwe hakitoweza kufahamika kutokana na kutolewa kiholela hasa pale kilipohusisha ugharamiaji wa siri wa operesheni zilizoendeshwa na magenge kihalifu ili kuongeza nguvu ya kumsaka.
Saa nyingi na zisizo na idadi zilizotumika kukesha kumsaka, yote haya hayakuwezesha au kusaidia kumkamata.
Ni harakati zilizoambatana na hisia za uongo, ubahatishaji na kutawaliwa na kila aina ya makosa ya kimkakati na kiufundi.
Itaendelea wiki ijayo