Na Seif Takaza, Iramba
MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Singida kwa kushiriki kikamilifu kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kumuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan apokee salamu za upendo kutoka kwa wananchi wa mkoa huo.
Dendego ametoa salamu hizo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Iramba, katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano yaliyofanyika katika viwanja vya  stendi mjini Kiomboi ambapo maadhimisho hayo yalifanyika Kimkoa.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema wakati wa maadhimisho hayo kuwa wananchi wa Mkoa wa Singida wanamshukuru Rais Dk. Samia kwa sababu wameendelea kupokea fedha nyingi wakiwemo wataalam kwa lengo la kuendelea kuwahudumia wananchi wa mkoa huo.
“Tunasema asante sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wewe na serikali unayoiongoza, imewasaidia sana wananchi katika Nyanja zote,” ameshukuru Dendego.
Pia, ameongeza kuwa wamepiga hatua kubwa kwa sababu wanapata maji safi na salama, hospitali, vituo vya afya, zahanati, shule na barabara za lami na katika Kilimo ambapo kutokana na juhudi za wakulima hao mkoa huo hauna njaa.
Kutokana na hayo, Dendego amewataka wananchi hao kuendelea kudumisha utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa kwa lengo la kuhakikisha siku zote wanakuwa salama.
“Ndugu zangu, mimi ni muumini wa kazi, mafanikio na furaha, hivyo ninataka watu wote ninaowaongoza wawe wanacheka na kufurahi tunapokutana, sitaki kuona machozi,” amesisitiza.
Dendego pia amempongeza Mkuu wa wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda kufuatia hali iliyojitokeza ya kutokupatikana mwananchi mwenye kero baada ya kiongozi huyo kutoa nafasi tatu kwa wanawake na nyinge tatu kwa wanaume.
“Mheshimiwa DC hongera sana, hii sio kawaida inaelekea unachapa kazi kweli kweli, endelea hivyo hivyo mdogo wangu, kazia hapo hapo hakuna kurudi nyuma,” amesema Dendego.
Kwa upande wa Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Elphas Luanji, amewataka wanachi hao kutembea kifua mbele kwa sababu serikali yao imeendelea kufanya mambo makubwa kwa ajili yao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano walizindua na kuweka kambi ya siku takribani tano ya Madaktari Bingwa na Bobezi katika hospitali ya wilaya hiyo ambaao walitoka Hospitali mbalimbali Rufaa Nchin.
Aidha, amesema kuwa katika kipindi cha muda huo mchache Madaktari hao Bingwa wameweza kuwaona na kuwahudumia wagonjwa 587 halikadhalika wamefanya upasuaji wa macho,mifupa na jumla kwa wagonjwa takriban 80.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kwa kweli kambi yetu imekua ya mafanikio makubwa sana, tulipokea wagonjwa kutoka Iramba na wilaya ya jirani ya Igunga mkoani Tabora,” amesema DC Mwenda.