LICHA ya Rais John Magufuli kupiga marufuku uagizwaji holela wa sukari kutoka nje ya nchi, lakini Bodi ya Sukari Tanzania imesisitiza ulazima wa kuagiza.
Akizungumza Dar es Salaam jana mbele ya Kamati ya Bunge ya Uwekezaji (PIC), Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Henry Semwanza, alisema kuna baadhi ya viwanda vimeishiwa na kwa sasa sukari iliyopo ni chini ya tani 40,000 ambayo haiwezi kukidhi mahitaji kwa kipindi hiki cha miezi isiyo ya uzalishaji.
“Lazima tukubaliane kwamba ni ukweli usiopingika kuwa nchi haijitoshelezi kwa uzalishaji wa sukari ya nyumbani na viwandani,” alisema Semwanza na kuongeza: “Sasa hivi akiba yetu ni chini ya tani 40,000, Kiwanda cha Kilombero kimeshafunga, Mtibwa kinatarajia kufungwa Aprili hii.”
Alisema katika uagizaji wa sukari wanazingatia sheria na taratibu licha ya kuwepo kwa baadhi ya waagizaji kukiuka masharti ya leseni ikiwamo kuingiza sukari nyingi kinyume na vibali vyao.
Alisema tatizo hilo linachangiwa na upakuaji wa sukari kufanywa na mamlaka nyingine tofauti na bodi na kwa kuwa baadhi ya watendaji kutokuwa waaminifu na wanaruhusu kuingizwa zaidi.
“Nipo tayari kuhukumiwa kama mtendaji ikiwa itagundulika kufanya vitu kinyume cha sheria kwa sababu sukari inayoagizwa lazima ipitishwe na baraza la mawaziri na wenyewe pamoja na wazalishaji ndio waliopitisha kwamba kwa mwaka huu ziingizwe tani 100,000 ili kufidia pengo katika kipindi cha Aprili hadi Juni ambacho wazalishaji wa ndani hawazalishi.
Pia alisema licha ya kuwa na malengo ya kuzalisha tani 600,000 kufikia mwaka huu, lakini imeshindwa na kujikuta wakizalisha tani 300,000 huku mahitaji yakiwa tani 420,000.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Ashura Luzi-Kihupi, alisema tayari wamepeleka maombi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambayo Rais Magufuli aliipa mamlaka ya kutoa kibali na muda wowote wataagiza kama ombi lao litakubaliwa huku akionya kuwepo kwa uhaba kama hawataagiza.
“Rais Magufuli alisema kama kuna ulazima wa kuagiza sukari kibali kinaweza kutolewa na Majaliwa na tumeshapeleka maombi na muda wowote tutaagiza,” alisema Kihupi.
Awali, wajumbe wa PIC walicharuka na kuilalamikia bodi hiyo kutofanya kazi yake ipasavyo na kusababisha uhaba wa sukari huku wakulima wadogo wa miwa wakipata shida ya soko kutokana na viwanda kukataa miwa yao.
Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Oran Njeza, alieleza namna bodi hiyo ilivyo na muundo mbovu na katika mpango mkakati wake wa mwaka 2010 yenyewe ilikiri hilo na kuazimia kuubadilisha lakini hadi sasa upo vile vile.
Naye Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftah Nachuma, alisema bodi hiyo inatakiwa kuvunjwa kwa kuwa imeshindwa kuhakikisha sukari ya kutosha inazalishwa nchini.
“Hii bodi ni jipu na inatakiwa kutumbuliwa kwa sababu wamepewa jukumu la kuhakikisha sukari inatosheleza lakini tangu ianzishwe haijawahi kufikia lengo hivyo inahitaji kuvunjwa,” alisema Nachuma.
Pia Makamu Mwenyekiti wa PIC ambaye ni Mbunge wa Busanda (CCM), Lolesia Bukwimba, alisema hawajaridhishwa na majibu ya bodi hiyo na inawapa muda wa kujiandaa na wataitwa tena kutoa maelezo ya kina.