32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mabula ambwaga Wenje kortini

mabulaNa Judith Nyange, Mwanza

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali shauri namba tatu la mwaka jana la kupinga matokeo ya ubunge lililofunguliwa na Ezekiel Wenje (Chadema) dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula, msimamizi wa uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akitoa uamuzi wa mahakama jana, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Kakusulo Sambo, anayesikiliza shauri hilo alisema baada ya kufungwa kwa kesi hiyo wakili wa mleta maombi, Deya Outa wa upande unaolalamikiwa aliwasilisha hoja kuijulisha mahakama hawana kesi ya kujibu kulingana na ushahidi ambao tayari umeshatolewa mahakamani na kuomba kesi hiyo kutupiliwa mbali.

Jaji Sambo alisema katika hoja iliyowasilishwa na upande unaolalamikiwa ilisema kuwa kiini katika shauri hilo ni Wenje aliyepata kura nyingi zaidi katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana na alitakiwa kulithibitisha hilo pasipo kuacha shaka lakini ameshindwa kufanya hivyo.

Jaji Sambo alisema shauri hilo lilijikita katika fomu namba 21B za vituo 693 vya uchaguzi vya Jimbo la Nyamagana na fomu hizo zilitakiwa kuwasilishwa mahakamani ndipo zifanyiwe kazi na kutolewa uamuzi na kukosekana kwa fomu hizo kunamaliza moja kwa moja shauri zima.

“Hakuna namna mleta maombi anaweza kuthibitisha madai yake bila kuwepo kwa fomu namba 21B za vituo 693 mahakamani, hoja zilizowasilishwa mahakamani na mawakili wa wajibu maombi wote zina mashiko, ushahidi uliopo mahakamani wa mashahidi watatu hauwezi kutengeneza kesi.

“Mahakama imejiridhisha kuwa wajibu maombi hawana kesi ya kujibu hivyo  shauri namba tatu la kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Nyamagana limetupiliwa mbali,” alisema Jaji Sambo.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, aliyekuwepo mahakamani wakati wa uamuzi huo ukitolewa aliambatana na Mabula na wanachama wa chama hicho hadi nje ya jengo la CCM Mkoa na kuzungumza na wananchi.

Mtaturu alisema wananchi wa Nyamagana waliuchoka upinzani ndiyo maana walimchagua Mabula kwa tofauti ya kura 1,900 na jana mahakama imejiridhisha ushindi huo ulikuwa halali na tafsiri yake ni kuwa hakuna ushindi wa mezani.

“Miezi mitano sasa tumekuwa na presha, tumepoteza muda mwingi na tumeingia gharama kwa sababu ya kesi hii, tumewaomba mawakili wao waandike gharama zote walizotumia katika kesi ili Wenje aweze kulipa,” alisema Mtaturu.

Mtaturu aliwahutubia wananchi hao walioandamana na Mabula hadi nje ya ofisi za CCM Wilaya ya Nyagamana na kusababisha Barabara ya Nyerere kufungwa kwa muda kupisha maandamano hayo.

Akizungumza na wananchi waliokuwa wamekusanyika nje ya ofisi hizo, Mabula aliwashukuru mawakili wake wote waliomtetea katika shauri hilo na chama chake kwa kumuunga mkono na kusema haki haipotei bali inachelewa na ameupokea uamuzi uliotolewa na mahakama kwa furaha.

Alisema ametumia nguvu, muda na fedha nyingi katika kesi hiyo na atakutana na mawakili wake kwa ajili ya kuangalia kiasi cha gharama watakazotakiwa kulipwa na fedha hizo atazielekeza katika vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.

“Gharama nitakayolipwa katika kesi hii nitaielekeza kwa vikundi vya ujasiriamali kama asante kwa kuendelea kuniunga mkono kipindi chote cha kesi, nimepoteza muda wa miezi mitano na kushindwa kufanya shughuli za maendeleo sasa nitafanya bila presha,” alisema Mabula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles