24.7 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Hapi aainisha mikakati mizito Jumuiya ya Wazazi

*Awataka wana-CCM kuziendea chaguzi kwa kujiamini

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

KATIBU Mkuu mpya wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania, Ally Hapi amesema atahakikisha anasimamia Jumuiya hiyo ili iwe yenye mvuto na kimbilio kwa kila mtu.

Akizungumza leo Aprili 8,2024 katika mapokezi yaliyoandaliwa Makao Makuu ya Jumuiya hiyo Dodoma, Hapi amesema Jumuiya hiyo inaenda vizuri hivyo ni lazima wahakikishe inakuwa ya kuvutia na inakuwa hai.

“Tunataka kujenga Jumuiya bora na iwe ya mfano na ambayo ni hai. Uhai wa Jumuiya ni vikao, tunataka vikao vifanyike nitazunguka na wenzangu kukagua, tuna wanachama wangapi.

“Jumuiya ya wazazi wanachama wake sio wazee, kanuni inazungumza kuanzia miaka 18 kwa sababu ni umri wa mtu mzima na anaweza kuwa na familia. Tunataka tuwavutie vijana wajiunge kwa wingi katika Jumuiya yetu,” amesema Katibu Mkuu huyo.

Amesema wanataka kuifanya Jumuiya hiyo kuwa imara na ambayo itakuwa kimbilio kwa kila mtu.

“Tunatamani tujijenge Jumuiya yetu iwe kimbilio kama kweli wanatukimbikia sawa lakini kama bado lazima tufungue milango, Je mipango yenu ipo wazi?

“Tutakutana kwenye kazi yako ndio itakayokutetea hatuwezi kukisaidia Chama chetu bila kufanya kazi,”amesema Hapi.

Katika hatua nyingine Hapi amemshukuru Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na vikao vya Halmashauri Kuu kwa kupitisha jina lake.

Hapi amewataka wanachama wa CCM kujiamini na wasiwe wanyonge kwani Chama hicho ni bora na kazi kubwa zimefanyika hivyo wanapokwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wajiamini.

“Tuelimishane mnakaa ndani mnajielimisha Serikali ya Rais Samia imefanya nini ilani lazima tukaisimulie kwa kujiamini tusiwe wanyonge.Maridhiano ni kujenga Demokrasia,mikutano unafanyika tunapoenda katika uchaguzi tunaenda katika uhalali wa kushika Dola.

“Twendeni kifua mbele,sisi tumesema muda wa huruma umeisha tunaenda kuitekeleza ilani,”amesema Hapi.

Amesema wamepewa jukumu la malezi, maadili afya hivyo jamii imekuwa na mmonyoko na ukatili, watoto wanabakwa hivyo ni lazima wasaidie kuhakikisha mambo yanakaa sawa.

“Nini nafasi yetu wazazi tuliopo katika Mikoa na Wilaya tunataka kuona Jumuiya ya Wazazi ikifuatilia kwa sababu watoto ndio Taifa la leo na kesho. Hili ni la kwetu kikanuni lazima tusimame vizuri kwa wazazi wote wa Tanzania.

“Kama ipo shule lazima ujue wanalelewa vipi haki imetendeka watuhumiwa wamepelekwa mahakamani haki itendeke, “amesema Hapi.

Kwa watendaji wa Jumuiya hiyo aliomba ushirikiano kuanzia ngazi ya Makao Makuu hadi Wilaya.

“Tuache hofu kwamba Katibu Mkuu ataniondoa katika nafasi yangu Mimi sijaja kuondoa watu kila mtu atimize wajibu wake

“Mimi sina kundi sio muumini wa majungu,makundi mimi ni muumini wa kazi,haki uadilifu na ukweli rafiki yangu ni kwenye haya,”amesema Katibu huyo.

Kwenye elimu amesema bado Kuna changamoto ya ajira ambapo amehoji Jumuiya inatimiza wajibu wake vipi kwa kuhakikisha vijana wanajiajiri.

Ameitaka Jumuiya kufanya shughuli za kijamii na penye dhulma ijipambanie isimamie.

“Tutakaa tupokee taarifa ya mali na watumishi na utendaji kazi wao na taarifa za uhai wa Jumuiya.Tunataka kuondoa ufanyaji kazi kwa mazoea,” amesema Hapi.

Pia, amewataka wana CCM kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles