27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa azungumzia uongozi wa JK

Pg 3NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu wa zamani ambaye pia alikuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Edward Lowassa, ameuchambua utawala wa Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.

Amesema pamoja na kazi aliyoifanya Kikwete kuliongoza Taifa, alijitahidi kuvutia wawekezaji japo kulikuwa na uzembe na ufisadi katika kuwasimamia.

Lowassa alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na wanazuoni wa ndani na nje ya nchi waliomtembelea nyumbani kwake, Masaki, Dar es Salaam.

Wanazuoni hao waliongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Lwekaza Mukandala.

“Jakaya kwa kiasi kidogo alijitahidi kuvutia wawekezaji japo kulikuwa na uzembe na ufisadi katika kuwasimamia,” alisema Lowassa.

Alisema kuwa si kweli kwamba kila mtu katika Serikali ya Jakaya alikuwa mlarushwa, ingawa ni kweli kwamba mfumo wa Serikali yake ulikuwa mbovu na wa kifisadi.

 

AMKOSOA MAGUFULI

Aidha, Lowassa amekosoa utendaji kazi wa Rais wa sasa, Dk. John Magufuli na kusema kwamba unamtia shaka kutokana na utaratibu wa uongozi wake.

“Hali ya siasa nchini hivi sasa ni ya hamasa, lakini isiyo na misingi endelevu kutokana na jinsi Serikali mpya inavyofanya kazi kwa ‘style’ mpya.

“Kwa kipindi kifupi, atakuwa maarufu, lakini hakuna mafanikio ya kiuchumi mbele ya safari. Kwa mfano, rais amekuwa akichukua maamuzi ya kugawa fedha wakati chombo cha kufanya hivyo kipo ambacho ni Bunge.

“Kugawa pesa si kazi ya rais, hiyo ni kazi ya taasisi kama Bunge ambalo lina mamlaka ya kuidhinisha bajeti,” alikosoa Lowassa.

Katika maelezo yake, Lowassa alisema anasikitishwa na hali ngumu ya maisha inayowakabili Watanzania na pia haridhishwi na idadi kubwa ya watu kuachishwa kazi.

“Ninasononeshwa ninapoona watu wanaachishwa kazi katika mashirika mbalimbali kwa sababu ya hali ngumu ya uendeshaji wa mashirika hayo.

“Bandarini sasa hivi nasikia uingizaji mizigo umeshuka kwa asilimia 50 baada ya kampuni nyingi za mizigo kufunga shughuli zake wakati pale kulikuwa na vijana wetu wengi waliokuwa wameajiriwa.

“Hao walioachishwa kazi, hivi sasa wako mitaani, kwa ujumla hali inatisha, maisha ya wananchi yanazidi kuwa magumu,” alisema Lowassa ambaye wakati wa Uchaguzi Mkuu alikuwa akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akizungumzia nchi wahisani, Lowassa alisema kitendo cha nchi hizo wakiongozwa na Marekani kusitisha baadhi ya misaada zikiwamo fedha za Changamoto ya Milenia (MCC), ni pigo kwa uchumi wa Taifa.

“‘Donors’ wamesitisha misaada, lakini sisi tunasema tunataka nchi ya viwanda, hivi fedha tutazitoa wapi kama si kuwategemea hao ‘donors’ wa ndani na nje kutusaidia katika hilo?

“Hawa ‘donors’ si watu wa kuwabeza, ‘they will pull us back’ (wataturudisha nyuma)… Hapa kinachotakiwa ni kufanya mabadiliko katika mfumo ili mfumo huo uwe endelevu,” alisema.

 

UCHAGUZI MKUU ULIOPITA

Kuhusu Uchaguzi Mkuu uliopita, Lowassa alizidi kusisitiza kwamba upinzani ulishinda, ingawa vyombo vya dola vilipora ushindi huo.
“Uchaguzi ule tulishinda na kila mtu anajua hivyo, hata Magufuli anajua hilo, lakini walitumia vyombo vya dola kupora ushindi wetu kwani zilinunuliwa pingu nyingi sana kuwafunga Watanzania walioamua kuleta mabadiliko,” alisema.

 

MIKAKATI 2020

Akizungumzia mikakati waliyonayo pindi watakaposhiriki Uchaguzi Mkuu mwingine mwaka 2020, Lowassa aliwaambia wanazuoni hao kuwa wamejipanga kuhakikisha hawaporwi tena ushindi.

“Tumejipanga kuhakikisha hatuporwi tena ushindi, kwa sababu hata joto la kutaka mabadiliko nchini bado ni kubwa kwa kuwa Watanzania wameichoka CCM,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles