25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 6, 2022

Contact us: [email protected]

Mbunge Chadema afariki dunia

Christina-Mugwai-LissuNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chadema kutoka Mkoa wa Singida, Christina Lissu Mughwai amefariki dunia kwa ugonjwa wa kansa.

Christina ambaye ni dada wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alifariki dunia jana   katika Hospitali ya Aga Khan,   Dar es Salaam alikokuwa amelazwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Lissu katika kundi la mtandao wa kijamii la WhatsApp wa wabunge wa Chadema, Christina  alikuwa akisumbuliwa na   kansa tangu mwaka jana.

“Waheshimiwa nawasalimu kutoka Kibondo. Nina habari zisizokuwa njema. Dada yangu na aliyekuwa Mbunge wetu wa Viti Maalum, Christina Lissu Mughwai amefariki dunia muda mfupi uliopita katika Hospitali ya Aga Khan.

“Alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa cancer (kansa) tangu mwaka jana. Niko nje ya Dar es Salaam na ndiyo kwanza taarifa hizi zimenifikia, sina taarifa zaidi juu ya mipango ya mazishi…tutawaarifu baada ya kushauriana na familia,”alisema Lissu.

Zitto atuma salamu

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe katika  salamu zake za rambirambi alizotuma katika ukurasa wake wa Facebook, alisema alipata kufanya kazi na Christina na kwamba aliipenda kazi yake, hivyo atamkumbuka daima.

“Christina Mughwai Lissu hatunaye. Nilibahatika kufanya kazi na dada Tina nikiwa Waziri Kivuli wa Fedha na yeye akiwa Naibu Waziri Kivuli. Tina ni msomi mzuri aliyependa kazi yake na ni mtu mwenye utulivu wa fikra.

“Natoa pole kwa familia nzima ya Lissu kwa msiba mkubwa uliowapata. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi,” alisema Zitto.

Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda (Chadema) alipiga simu chumba cha habari MTANZANIA akieleza kusikitishwa na taarifa hizo za kifo cha Christina.

“Ni rafiki yangu mpambanaji, alijua kupangilia hoja zake bungeni, alikuwa akinipa moyo kabla sijawa mbunge.

“Aliniambia kupigania haki za wanyonge si kazi ya siku moja inahitaji ujasiri na kujitoa kwa niaba yao. Ametangulia kamanda Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi Amina,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu Bara (Chadema), Salum Mwalimu, alipopigiwa simu aliomba apewe muda  awasiliane na viongozi wenzake wa chama hicho kwa sababu hakuwa na taarifa zozote kuhusu kifo hicho.

“Ndiyo kwanza taarifa hizo nazisikia kwako, nipe muda kidogo niwasiliane na wasaidizi wangu   na viongozi wengine, nitakupa taarifa,” alisema Mwalimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,606FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles