CHRISTINA GAULUHANGA NA GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM
KAMATI ya Bunge ya Katiba na Sheria, imeagiza Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kusitisha miradi yote mipya hadi hapo itakapopitia ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kujiridhisha kama haina harufu za rushwa.
Akisoma taarifa ya majumuisho ya ziara ya wajumbe wa kamati hiyo waliyoifanya katika taasisi mbalimbali za Serikali, ofisi za mawaziri na mahakama jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kupitia miradi iliyopita na kubaini taarifa zake hazijajitosheleza.
“Tumepita wilaya mbalimbali, taasisi za Serikali na kuandaa mapendekezo yetu kama kamati, ikiwamo hili la kusitisha miradi yote mipya ya NSSF hadi hapo tutakapopitia ripoti za CAG,” alisema Mchengerwa.
Alisema kamati inataka kujiridhisha kama kiwango cha fedha kilichotengwa katika miradi hiyo kipo sahihi.
Mchengerwa alisema baadhi ya miradi waliyoitembelea ni pamoja na ujenzi wa nyumba eneo la Kijichi na daraja la Kigamboni.
Alisema kamati imetoa maelekezo kwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA) kuangalia miradi inayoanzishwa na mashirika wanayoyasimamia pamoja na sera ya uwekezaji.
“Ni vyema tukajiridhisha kama mchakato wa uanzishwaji miradi, ushauri wa kitaalamu umekidhi matakwa,” alisema Mchengerwa.
Aliongeza kuwa zipo nyumba nyingi za mradi ambazo hazina wapangaji, hivyo ni vyema ikafanyiwa uchunguzi kama miradi hiyo ilianzishwa kwa ajili ya kupata asilimia kumi.
“Ipo haja ya kupitia mchakato wa miradi hii ili kuona kama sera ilifuatwa,” alisema Mchengerwa.
Alisema wameiomba Serikali iwasilishe mbele ya kamati hiyo ripoti ya CAG kuhusu mashirika hayo ili waweze kutoa mapendekezo kama yana upungufu na hatua za kuchukua.
Wakati huohuo, Mchengerwa alisema wameipa wiki mbili Serikali kuhakikisha inakabidhi taarifa sahihi za ujenzi wa jengo la ofisi ya Makamu wa Rais ambalo kabla kufunguliwa linaonekana limechakaa.
Alisema cha kusikitisha asilimia 98 ya malipo ya jengo hilo tayari yamefanyika, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Mchengerwa alisema kamati imeagiza CAG afanye ukaguzi ili kubaini fedha zilizotumika kama zinalingana na thamani ya jengo.
Kamati hiyo pia imeitaka SSRA kutatua tatizo la ofisi za kudumu haraka iwezekanavyo, kwani tangu waanze kupanga mwaka 2008 hadi sasa wametumia Sh bilioni 4.5 kulipia pango.
Alisema kila mwaka mamlaka hiyo inatumia Sh milioni 600, hivyo ni jambo jema kuanzia sasa watafute sehemu ya kujenga ofisi ya kudumu.