28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Elinino kupungua nguvu msimu wa masika

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema hali ya El – Nino inayoendelea katika Bahari ya Pasifiki itapungua nguvu katika msimu wa mvua za masika zinazotarajiwa kuanza wiki ijayo.

Msimu wa mvua za masika ambazo zitaanza wiki ya nne ya Februari ni mahususi kwa Mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Unguja na Pemba, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na Kigoma.

Akizungumza leo Februari 22,2024 wakati akitoa taarifa za mwelekeo wa msimu wa mvua wa masika Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Ladslaus Chang’a, amesema mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Amesema athari zinazotarajiwa ni vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko na kuathiri ukuaji wa mazao, kuongezeka kina cha maji katika mito na mabwawa na magonjwa ya mlipuko kutokana na uchafuzi wa maji.

“Vipindi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi na kupelekea uharibifu wa miundombinu, mazingira, upotevu wa mali na maisha.

“Mamlaka husika katika idara mbalimbali na idara ya menejimenti ya maafa zinashauriwa kuendelea kuratibu utekelezaji wa mipango itakayosaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza,” amesema Chang’a.

Kaimu mkurugenzi huyo amesema magonjwa kama vile ukungu (fungus) yanatarajiwa kuongezeka na kuathiri mazao kama nyanya, ufuta, maharage na mazao jamii ya mizizi.

Mamlaka hiyo imewashauri wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalili na kutumia pembejeo husika kwa wakati, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani.

Kulingana na TMA, magonjwa ya mlipuko yanaweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa miundombinu ya maji na kushauri mamlaka husika kuchukua tahadhari ili kupunguza athari za kiafya kwa kuharibu mazalia ya mbu, kutibu maji kabla ya kuyatumia na kuhakikisha uwepo wa vifaa tiba vya kutosha katika vituo vya afya.

Akizungumzia namna walivyojipanga kukabili changamoto zitakazotokana na mvua hizo Wakala wa Barabara na Vijijini (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam umesema umejipanga kutatua changamoto zitakazojitokeza kwa haraka.

“Tunawaasa wananchi waepuke kutumia mitaro kama jalala kwa sababu wakiiziba itakuwa ni changamoto kubwa,” amesema Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam, Geofrey Mkinga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles