25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Wananchi waliovamia shamba la Wizara ya Mifugo wapewa saa 24 kuondoka

Na Gustafu Haule,Pwani

WANANCHI waliovamia shamba la Mitamba kiwanja namba 34 linalomilikiwa kisheria na Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo Kata ya Pangani katika Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kuondoka mara moja katika eneo hilo ndani ya saa 24  kwakuwa uendelezaji wowote waliohufanya ni batili.

Kiwanja hicho chenye ukubwa wa hekta 1,037 sa na ekari 2,592.5 kinamilikiwa kisheria na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa hati miliki na mpaka sasa kimevamiwa na wananchi kinyume na sheria.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Mhandisi Mshamu Munde, ameweka bayana suala hilo Januari 8, mwaka huu katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake kuwa muda wowote kuanzia sasa tingatinga litaingia eneo hilo kusafisha kila kitu.

Munde amesema kuwa kiwanja namba 34 ni sehemu ya eneo lenye ukubwa wa hekta 4,000 sawa na ekari 10,000 ambalo lilitwaliwa kisheria na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kulipa fidia wananchi waliokuwa wakimiliki eneo hilo kiasili na jumla ya wananchi 1,556 walilipwa fidia yao kwa awamu nne ikiwa kuanzia mwaka 1988 mpaka 1991.

Amesema baada ya wizara kulipa fidia, eneo hilo lilipimwa na kumilikishwa kiwanja namba 34 ambapo hata hivyo baadhi ya wananchi walivamia na kuuza sehemu ya kiwanja hicho na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Aidha, kutokana na vitendo vya uvamizi kuongezeka katika eneo hilo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliyekuwepo wakati huo, William Lukuvi alifanya mkutano wa hadhara Julai 15, 2021 katika Kata ya Pangani Mtaa wa Lumumba.

Kwa mujibu wa Munde, mkutano huo uliwahusisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani, uongozi wa Halmashauri ya Mji Kibaha pamoja na wananchi waliovamia eneo hilo.

Mkurugenzi huyo amesema, Waziri Lukuvi katika mkutano huo alitoa agizo kwa wananchi kuacha kuvamia na kuuza eneo hilo kwakuwa ni mali halali inayomilikiwa kisheria na wizara hiyo.

Aidha, pamoja na maelekezo ya zuio hilo lakini pia Waziri Lukuvi aliunda kamati maalum ya uchunguzi wa kina kuhusu uvamizi uliofanywa ndani ya kiwanja namba 34 na hatimaye kamati hiyo iliundwa Julai 15,2021.

Munde, ameongeza kuwa kamati hiyo ilipomaliza kazi yake iliwasilisha taarifa na mapendekezo kwa Waziri Lukuvi na Dk. Angelina Mabula ambaye kwa wakati huo alikuwa Naibu Waziri pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi wa wakati huo, Mashimba Ndaki.

Amesema ikawa haitoshi mawaziri hao kwa pamoja walifanya mkutano wa hadhara Septemba 2, 2022 katika kata ya Pangani Mtaa wa Lumumba, mkutano huo ulikuwa na lengo la kutoa taarifa ya kamati kwa wananchi na kisha mawaziri hao kukabidhi kwa Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya usimamizi na utekelezaji.

Munde anaeleza kuwa baada ya maagizo ya Mawaziri kupokelewa na Mkuu wa Mkoa, Halmashauri ilitoa notisi mara mbili ambapo ya kwanza ilikuwa ya siku saba na ilitolewa Novemba 22,2022 na notisi ya pili ya siku 14 ilitolewa Novemba 23,2023 lakini wananchi hawakutii agizo hilo.

Amesema Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge naye alifanya mkutano wa hadhara Kata ya Pangani mtaa wa Lumumba Oktoba 13,2023 na kutoa maagizo kwa Halmashauri ya Mji Kibaha na Taasisi za serikali ndani ya mkoa kuhusu mpango wa uendelezaji wa kiwanja namba 34 .

Amesema miongoni mwa maagizo hayo ni kuwa kwakuwa kiwanja namba 34 Pangani kimepimwa na kinamilikiwa kisheria na Wizara ya mifugo na uvuvi, wavamizi wote waliofanya maendelezo ikiwemo kujenga nyumba zao ndani ya eneo hilo hawana uhalali hivyo uendelezaji wao ni batili.

Agizo lingine ni pamoja na kuhakikisha hatua za kinidhamu zinachukuliwa dhidi ya viongozi wa m mitaa, watendaji wa mitaa na wataalamu waliohusika katika kusaini na kupitisha mauziano ya ardhi katika kiwanja hicho .

Amesema kufuatia maagizo hayo kwasasa Halmashauri ya Mji Kibaha imefika mwisho na sasa tayari wameweka mpango maalum wa uendelezaji wa kiwanja hicho na kwamba hakunabudi wananchi kuondoka.

“Ndani ya masaa 24 tutaanza zoezi la kusafisha eneo la kiwanja namba 34, kwahiyo wavamizi wote waondoe mali zao wenyewe kwa hiari yao maana kama wataendelea kukaidi sisi tukipita hatutaacha kitu maana tunaanza na mpango wa uendelezaji,” amesema Munde.

Hata hivyo, Munde amesema kuwa katika eneo hilo yapo maeneo ambayo hayajaguswa lakini kwa wale ambao wameguswa na wamepewa notisi ya kuondoka kupitia viongozi wa serikali za mitaa wamefika kaya 130.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles