Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA),imefanya ukaguzi katika maduka ya dawa na kunasa wachepushaji wa dawa za serikali, huku ikiwaonya wasambazaji na wauza dawa bandia.
Imetaja mikoa vinara kwa uchepushaji wa dawa za serikali kuwa ni Dar es Salaam, Lindi na Simiyu.
Akizungumza wakati WA kutoa taarifa ya operesheni ya ukaguzi waliofanya mbele ya waandishi wa habari leo Desemba 20,2023 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo, amesema dawa na vifaa tiba bandia ni hatari kwa afya ya jamii.
Amesema opereshemi maalumu ya kukamata dawa bandia, vifaa tiba na vitendanishi vya serikali, zisizo na usajili na dawa za kulevya iliyofanyika Novemba 20 hadi 24,2023.
“Operesheni hii ilifanyika kwa wilaya mbalimbali zilizopo katika mikoa 13 ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro, Kigoma, Katavi, Mwanza, Simiyu, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Songwe, Lindi na Ruvuma,” amesema.
Amesema ukaguzi huo ulilenga bidhaa bandia za afya katika hospitali, vituo vya afya zahanati, maghala, maduka ya jumla na rejareja ya watu binafsi na maeneo mengine yasiyo rasmi.
Ameeleza kuwa bidhaa za serikali zilizokutwa zinauzwa katika maduka ya dawa na vituo binafsi vya kutolea huduma ni dawa za mseto ya kutibu malaria ya vidonge aina ya ALU, dawa la mseto ya kutibu kifua kikuu, dawa za uzazi wa mpango.
Amesema dawa hizo zilikutwa katika maduka yaliyoko mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Ruvuma na Simiyu.
“Vifaa tiba vya serikali vinavyokadiliwa kuwa na thamani ya Sh milioni 11.297 vilikamatwa katika vituo na maduka binafsi na baadhi ni vifaa vya kupima malaria na virusi vya ukimwi,” amefafanua.
Amesema katika operesheni hiyo walikamata dawa zilizokwisha muda wa matumizi zenye thamani inayokadiriwa kuwa Sh milioni 9.5 ambazo zilikamatwa zikiwa hazijatengwa kwa mujibu wa utaratibu katika kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa Mashariki na Nyanda za Juu Kusini.
Amesema dawa bandia za binadamu zenye thamani ya Sh milioni 5.9 zilikamatwa Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Magharibi na Kanda ya Juu Kusini ndiyo inaongoza ikifuatiwa na Magharibi.
Fimbo amesema jumla ya bidhaa zenye thamani ya Sh milioni 172.2 zimekamatwa katika operesheni hiyo.
Pia amesema operesheni hiyo ilibaini uwepo wa dawa zenye madhara ya kulevya aina ya ‘pathidine’ katika maeneo mbalimbali zikiuzwa kwa siri na mtandao wote umebainika na wahusika wameshafahamika.
Aidha amesema watuhumiwa wote waliokutwa na kuhusika moja kwa moja na kusambaza au kuuza dawa, vifaa tiba au vitendanishi vya serikali na bandia wamefikishwa katika vyombo vya sheria.
Amesema jumla ya majalada 13 yamefunguliwa dhidi ya watuhumiwa na taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea katika vituo vya polisi.
“Jumla ya Sh milioni 100 zimetozwa kama faini kwa wote ambao makosa yao hayakuhitaji kufikishwa mahakamani,” amesema.
Ametaja hatua yingine iliyofanyika ni kuondoa dawa bandia, dawa na vifaa tiba duni, dawa na vitendanishi vilivyokwisha muda wa matumizi na dawa zisizosajiliwa katika soko kwa ajili ya taratibu za uteketezaji kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Pia wametaifisha dawa na vifaa tiba vya serikali na kuelekeza wamiliki wa maduka yasiyo na vibali na wataalamu kufunga maduka yao na kufanya utaratibu wa kuyasajili rasmi.
Fimbo amesema serikali itaendelea kuwatafuta na kuwachukulia hatua wale wanaofanya biashara hiyo haramu kwa mujibu wa sheria ya dawa na vifaa tiba.
“Wale wote wanaotengeneza, kusambaza, kuuza dawa, vifaa tiba na vitendanishi bandia kuacha mara moja kwani ni hatari kwa afya ya jamii kwani bidhaa kama hizo zinakosesha watu haki yao ya kupata huduma ya matibabu kuweza kupona maradhi yao,”amesema.
Amewataka watoa huduma za afya kwa hospitali kuacha kuiba dawa, vifaa tiba, vitendanishi vya serikali na kuviuza katika maduka ya watu binafsi.
Naye Msajili wa Baraza la Famasia, Elizabeth Shekalaghe ameonya maduka ya dawa yanayotoa huduma kinyume kama kuchoma watu sindano kwani kufanya hivyo kunahatarisha afya za wananchi.
“Nawataka wananchi kutoweka afya zao rehani kwa kwenda katika maduka ya dawa kuchukuliwa vipimo, kuchomwa sindano kwani hayaruhusiwi kutoa huduma hiyo.
“Kazi ya duka la dawa ni kuuza dawa pekee na kazi ya maabara ni kupima tu na sio kutoa dawa nawasihi wananchi kuweni makini kwa hili,” amesema.