Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Wizara, idara na taasisi za serikali zimeanza kuweka shughuli za kifua kikuu katika mipango kazi yao ili kuwafikia wananchi ambao ni walengwa.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati wa uzinduzi wa Mpango wa uwajibikaji wa kisekta wa mapambano dhidi ya kifua kikuu (MAF – TB).
Mpango huo ulibuniwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2018 kwa ajili ya kuratibu ushiriki wa sekta na wadau katika kutokomeza kifua kikuu ifikapo 2030.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ambapo Mratibu wa Mawasiliano wa mpango huo, Isabela Chilumba, amesema wameanza kujenga uwezo katika ngazi zote za wizara hiyo kuhusu mpango huo.
Akizungumza Novemba 23,2023 wakati wa mkutano kuhusu utekelezaji wa MAF – TB, Chilumba amesema; “Tumeanzisha mpango kazi mdogo ili kujenga uwezo katika ngazi zote za Wizara ya Ardhi kulingana na muundo mpya wa wizara…changamoto kubwa ni uelewa katika jamii.
Naye Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Seif Mbarouk, amesema wameanza kuwaashirikisha wadau mbalimbali na kupanga mikakati maalumu ya kutokomeza ugonjwa huo.
“Tutakutana na sekta nyingine kama ya usafirishaji kwa sababu kumekuwa na changamoto ya msongamano wa watu katika vyombo vya usafiri zikiwemo daladala, mabasi ya mwendokasi na treni, tukikaa nao pamoja tutaweza kuweka mikakati maalumu ya kupambana na kifua kikuu ili kufikia malengo ya kukitokomeza ifikapo mwaka 2030,” amesema Dk. Mbarouk.
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dk. Catherine Saguti, amesema wanafanya uchunguzi wa kifua kikuu mara kwa mara kwa watu anaoingia katika manispaa hiyo wakiwemo wanaopitia Stendi ya Magufuli kwa kutumia gari la kliniki tembezi ambalo pia lina X – ray kubwa ya kugundua wadudu wa ugonjwa huo.
Mratibu Uraghibishi na Mawasiliano Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma, Julius Mtemahanji, amesema malengo ya Serikali ni kutokomeza kifua kikuu na kuwa na wagonjwa chini ya 10 kati ya watu 100,000.
Takwimu za Serikali za mwaka 2022 zinaonyesha kwa sasa kuna wagonjwa wapya 128,000 sawa na asilimia 64 ya wagonjwa wote waliotarajiwa kugundulika kutokana na makisio ya WHO lakini asilimia 36 bado hawajatambulika.
“Kila mgonjwa mmoja ana thamani kubwa kwa sababu tusipompata anaendelea kuambukiza wengine,” amesema Mtemahanji.
Aidha amesema kwa mwaka 2021 vifo kutokana na ugonjwa huo vilikuwa 26,800 sawa na vifo 71 kwa siku.