Na Mwandishi wetu, Tanga
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),  Mhandisi Mohammed Besta,  kukamilisha usanifu wa barabara ya Mkata- Kwamsisi ya kilomita 36, ifikakapo Disemba 31, 2023.
Akizungumza katika ziara yake ya kukagua athari za mvua za vuli mkoani humo leo Novemba 24, 2023, Bashungwa amesema fedha za mradi huo zipo tayari hivyo kinachotakiwa ni kazi ya usanifu ifanyike haraka ili ujenzi uanze mara moja.
“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameashatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii, hivyo kazi ya usanifu ikikamilika ujenzi uanze haraka,” amesisitiza Bashungwa.
Amezungumzia umuhimu wa watendaji wa TANROADS wa ngazi zote kushirikiana na mamlaka za serikali ya mitaa ili kurahisisha ufuatiliaji wa kazi za wakandarasi na kuwezesha kufutilia haki za watumishi katika miradi ya ujenzi.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Besta amesema wamejipanga kuhakikisha usanifu unakamilika kwa wakati na taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi huo unakamilika mapema iwezekanavyo.
Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amemuonya vikali mkandarasi wa kampuni ya kutoka China anaejenga barabara ya Mkange-Tungamaa-Pangani yenye urefu wa kilomita 120.8 kuhakikisha anaongeza kasi kwani serikali haitavumilia utetezi wowote unaochelewesha.
“Gharama za ucheleweshwaji wa ujenzi wa barabara serikali haitavumilia mkandarasi yoyote atakayechelewesha mradi.
“TANROADS endelea kuwahimiza wakandarasi na wasimamizi wa miradi ambao hawakamilishi kazi kwa wakati wasipewe kazi nyingine,”amesema Bashugwa.